Walimu
wa Shule ya Sekondari Hasanga, iliyopo wilayani Mbozi mkoani Songwe na
wafanyabiashara wawili, wanahojiwa na vyombo vya usalama mkoani Mbeya
kwa tuhuma za kuhusika na utengenezaji wa mitihani feki ya kidato cha
nne.
Watuhumiwa
hao, James Kapinga (36) ambaye anadaiwa kufanya kazi Shule ya Sekondari
ya Hasanga pia anajitolea kufundisha Shule ya Sekondari ya Wazazi ya
Sangu, Baraka Mwazambe (28), mfanyabiashara na mkazi wa Tunduma na
mtaalamu wa masuala ya Tehama (IT), Alex Mochi.
Watu
hao kwa pamoja inadaiwa walikamatwa juzi usiku baada ya mwanafunzi
mmoja ambaye jina lake na la shule vimehifadhiwa kukutwa na mtihani wa
somo la Kiingereza na alipobanwa, inadaiwa aliwataja wahusika hao.
“Mwanafunzi
huyu ni wa shule nyingine tena si ya Mbeya, alikutwa na mtihani feki wa
somo la Kiingereza, alipohojiwa alieleza mtihani huo ulitoka Mbeya na
Serikali ilipofuatilia iliwabaini wahusika ambao walikuwa wanasambaza
mitihani feki,” kilisema chanzo kimoja cha habari hii.
Akizungumzia
sakata hilo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariamu Mtunguja, alikiri
ofisi yake kupokea taarifa juu ya uvujaji wa mitihani na walipofuatilia
walibaini mitihani hiyo ni feki.
“Mbeya
hakuna mitihani iliyovuja kama inavyoelezwa katika mitandao, ukweli ni
kwamba suala hilo lilifuatiliwa ilibainika mitihani inayosambazwa si ile
iliyochapishwa na Baraza la Mitihani la Taifa, ni feki na baadhi ya
wahusika wanahojiwa na vyombo vya dola,” alisema.
Naye Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Mbeya, Benedict Sandy, alisema hakuna mitihani iliyovuja.
“Mitandao
imekuwa ikitoa taarifa za upotoshaji eti mitihani imevuja, mitihani
iliyosambaa na kukutwa na baadhi ya wanafunzi tena si wa Mkoa wa Mbeya
ni feki na wahusika wanaodaiwa kuisambaza wamekamatwa.
“Nawaomba
wanafunzi wazingatie yale waliyofundishwa, mitihani hiyo inakuja kwa
lengo baya la kuwapotezea muda wao na mwisho wa siku kuishia kufeli,
watu wanaofanya kazi hiyo wapo kimasilahi,” alisema.
Post a Comment