Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu raia watatu wa Pakistan, kifungo cha
miaka minne jela au kulipa faini ya Sh milioni 125 baada ya kupatikana
na hatia ya kuingilia mtandao wa mawasiliano na kuisababishia serikali
hasara ya Sh milioni 145.
Hakimu
Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage, alitoa hukumu hiyo baada ya washtakiwa,
Hafees Irfan, Mirza Irfan Baig na Mirza Rizwani Baig, kukiri makosa yao.
Akitoa
adhabu hiyo, Hakimu Mwijage alisema, washtakiwa wamepatikana na hatia
ya makosa manne na katika kila kosa watalipa faini ya Sh milioni tano au
kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela, ambayo ni sawa na faini ya Sh
milioni 20 au kifungo cha miaka minne jela.
Aidha,
alisema kwa sababu mashtaka yanahusisha kuisababishia hasara Mamlaka ya
Mawasiliano (TCRA), kila mshtakiwa anatakiwa kulipa faini ya Sh milioni
35, pia washtakiwa wakimaliza kutumikia vifungo vyao, warud ishwe
nchini kwao na vifaa walivyokutwa navyo vitakuwa mali ya serikali.
Awali,
kabla ya hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Esther Martin aliwasomea
washtakiwa hao maelezo ya awali na kudai kuwa katika tarehe tofauti, Dar
es Salaam, washtakiwa walikutwa na vifaa vya kuunganishia mawasiliano
ya kimataifa bila kuwa na kibali cha TCRA.
Alidai,
washtakiwa walitoka Pakistan na kwenda maeneo mbalimbali ikiwemo Arab
Emirates, Malaysia, Msumbiji kwa ajili ya kutumia vifaa hivyo, pia
waliingia nchini katika tarehe tofauti na kufikia kwenye chumba namba
905 katika Hoteli ya Butterfly iliyopo Kariakoo, Dar es Salaam.
Inadaiwa
wakiwa kwenye chumba hicho, waliunganisha mawasiliano kwa kutumia vifaa
vya kimataifa bila kuwa na kibali cha TCRA, lakini wakati wakiendelea
na kazi zao ilibainika kuwa, kuna watu katika maeneo hayo wanatoa huduma
ya mawasiliano, kinyume cha sheria.
Aliendelea
kudai kuwa, Oktoba 5, mwaka jana, maofisa wa Polisi wakiambatana na
TCRA walifika maeneo hayo na kufanya upelelezi, kisha wakawakamata
washtakiwa hao katika hoteli wakiwa na vifaa mbalimbali vya mawasiliano,
ambavyo ni kadi za simu 273, CPU 18, Laptop saba, Moderm ya Huawei na
vocha zilizokwishatumika.
Washtakiwa
walifikishwa kituo cha Polisi Kijitonyama na baada ya kufanya
upelelezi, ilibainika kuwa wameisababishia serikali na TCRA hasara ya Sh
milioni 140.
Baada
ya kusomewa maelezo yao, washtakiwa walikiri makosa. Wakili Esther
aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa washtakiwa ili iwe fundisho kwa
wengine na makosa hayo, yasiwe yanajirudia rudia, adhabu itolewe kwa
kuzingatia hasara walioisababisha washtakiwa, pia alidai makosa hayo
yanahatarisha usalama wa taifa.
Hata
hivyo, Wakili wa utetezi, Shadrack Ishengoma aliiomba mahakama hiyo
kuwapunguzia adhabu hiyo washtakiwa kwa sababu wamekiri makosa yao, pia
wanategemewa na familia zao, na kuongeza kuwa washtakiwa wameshakaa
rumande kwa miezi 13 yaani zaidi ya mwaka mmoja.
Hakimu Mwijage alisema ametoa adhabu hiyo kwa kuzingatia hoja za pande zote mbili na washtakiwa walilipa faini na kuachiwa.
Post a Comment