Bunge la Jamhuri ya Muungano jana
liliweka kando tofauti zao za kisiasa wakati lilipowaweka kwenye kibano
mawaziri watano kutokana na utendaji wao.
Wabunge wa chama tawala na upinzani walionyesha makali yao wakijadili Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2017/18 na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao, ikiwa ni mwaka mmoja tangu Serikali ya Rais John Magufuli iingie madarakani.
Mbali na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk
Philip Mpango, mawaziri wengine waliowekwa kwenye hali ngumu ni Ummy
Mwalimu, ambaye ni Waziri wa Afya, Angellah Kairuki (Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais-Utumishi), Charles Mwijage (Viwanda, Biashara na
Uwezeshaji) na Profesa Joyce Ndalichako (Elimu, Sayansi na Teknolojia).
Mwongozo huo wa mpango wa kuandaa bajeti unaonyesha Serikali itatumia
Sh32.9 trilioni kwa mwaka ujao wa fedha, ikiwa ni ongezeko la Sh3.4
trilioni kulinganisha na bajeti ya mwaka huu.
Mjadala wa wabunge hao
ulijielekeza katika kuchambua utendaji wa mawaziri hao na hali ilivyo
kwenye wizara zao, hasa kiuchumi ambayo inaelezwa kuwa ngumu kutokana na
wananchi kudai fedha zimepotea kwenye mzunguko.
Aliyefungua
mashambulizi hayo ni mbunge wa Busega (CCM), Dk Raphael Chegeni
aliyesema Dk Mpango ni msomi, lakini ana “kiburi, si msikivu na hataki
kushauriwa”.
Dk Chegeni alisema wabunge walimshauri mambo mengi waziri
huyo katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2016/17, lakini
hakutaka kusikiliza na ndiyo maana hali imekuwa ngumu kila eneo.
‘’Dk
Mpango unapaswa kuwa msikivu na kuacha kiburi. Tunayokushauri yachukue
(kwa kuwa) tunakusaidia ufanye kazi.Tulikuambia mambo mengi,
ukatudharau sasa yanatokea, kila kona hakuna unafuu,’’ alisema.
Dk
Chegeni alisema uchumi ambao anauzungumziwa kwenye mpango wake hauendani
na hali halisi ya maisha ya wananchi, akisema hata halmashauri
hazijapewa fedha hadi sasa.
“Wananchi hawana fedha, wabunge hawana
fedha. Fedha ambazo Mamlaka ya Mapato (TRA) inaeleza kuwa inakusanya,
ziko wapi wakati madeni yameongezeka?”
Alimtaka waziri huyo kutimiza wajibu
wake kwa unyenyekevu na kwa kusikiliza ushauri wa wabunge kuhusu wizara
yake.
“Umekuwa
ni tatizo sana. Hata ukiitwa na jumuiya za
wafanyabiashara huendi, ukiitwa na kamati ya Bunge ya Bajeti
huendi.Umekuwa mgumu kupatikana, dhamana uliyopewa ni kubwa, usitumie
vibaya
mamlaka yako,” alisema Dk Chegeni.
Mbunge mwingine aliyechangia
alikuwa John Heche (Tarime Vijijini-Chadema), ambaye alisema mtu wa pili
kutumbuliwa na Rais John Magufuli baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya
Ndani, Charles Kitwanga atakuwa Dk Mpango.
“Kwa sababu gani utakuwa ni
wa pili kutumbuliwa? Kwa sababu mambo yanapokwama, mipango yote
mliyopanga inapokwama, wewe ndiye unabebeshwa zigo hilo ili yeye
aonekane yuko sawa wakati mnakosea wote,” alisema.
Heche alisema
wamesimamisha ajira kutafuta watumishi hewa kwa mwaka mzima, lakini wako
vijana waliosomeshwa na baba zao wako mitaani kwa kukosa ajira.
“Dada
zetu wanajiuza, mikopo nayo hakuna, mnatafuta wanafunzi hewa. Kilimo
nako mnatafuta wakulima hewa. Cha msingi mseme kuwa Serikali yenu
imefilisika na hamuwezi kutekeleza kitu chochote, msaidiwe,” alisema.
Mbunge wa Solwa (CCM), Ahmed Salum aliwataka wabunge wa CCM kumwambia
ukweli Dk Mpango kuwa wanakwenda kugonga mwamba katika uchumi.
“Unajiuliza fedha zimekwenda wapi? Unakuja hapa unasema kuwa uchumi umekua, how (kwa vipi)?
Twiga imeshakuwa taken over (imeshachukuliwa), CRDB imetangaza hasara na
TIB hasara,” alisema.
Alisema hali hiyo inaonyesha kuwa baada ya miaka
miwili benki hizo zinakwenda kufungwa na huo utakuwa ni mgogoro wa
kiuchumi nchini.
Alisema hilo huenda linatokana na mawaziri kutokwenda
kuomba kura na hivyo hawafahamu joto la maisha lililopo kwa wananchi
majimboni.
“Mimi natoka Jimbo la Solwa, unaahidi, unadanganya hadi
unachoka. Alikuwa JK ameondoka, anakuja Magufuli ataondoka hakuna
lililofanyika,” alisema.
Aliitaka Serikali kurejesha fedha za mifuko ya
hifadhi ya jamii ilizoziweka “kabatini” Benki Kuu na mifuko hiyo iziweke
fedha hizo kwenye benki za biashara ili fedha zianze kuzunguka.
Aliitaka Serikali kulipa madeni ya ndani ili fedha zianze kuzunguka na
kwamba kumekuwa na joto hata ndani ya Bunge, akisema kuna ukata.
Salum
alisema makusanyo ya kodi yanayotangazwa na kuonekana kuwa makubwa
yanatokana na watu kulipa madeni ya nyuma na mara baada ya kuisha kwa
malimbikizo hayo, makusanyo yatabaki kama ilivyokuwa wakati wa Serikali
ya Awamu ya Nne.
“Watalipa itafika mahali itakwisha na kubaki na
makusanyo ya siku hiyo, cash revenue (fedha taslimu). Hapo ndipo
itashuka kutoka Sh1.5 trilioni hadi Sh800 bilioni iliyoachwa na Rais
Jakaya Kikwete,” alisema.
“Haya madeni yakiisha tutarudi kukusanya
bilioni. Hatuwezi kufika trilioni hizo za leo. Tuna matatizo. Kipindi
cha Kikwete, TRA ilikuwa inakusanya Sh850 bilioni, lakini nchi ilikuwa
nzuri na mambo mengi yalienda vizuri kuliko sasa.”
Alisema Rais Magufuli
amekuwa na maono mazuri ya kuifanya nchi kufikia mafanikio ya Thailand,
lakini tatizo wasaidizi wake hawamwambii ukweli ama wanaogopa
kufukuzwa.
“Magufuli tulikuwa naye hapa kwa zaidi ya miaka 10,
namfahamu. Ukienda na data (takwimu) ukamueleza kukimbiwa na
wafanyabiashara bandarini, atakuelewa,” alisema.
Mbunge wa Nzega Mjini
(CCM), Hussen Bashe alisema mipango ya Dk Mpango haifanani na ahadi
walizozitoa kwa wananchi kuwa watawaboreshea hali ya uchumi
watakapowachagua.
“Kwa sababu kaka yangu (Dk Mpango) hujaenda kuomba
kura? Dunia imebadilika tunaenda kufa tunapaswa kubadilika,” alisema
Bashe.
Alisema miradi mingine kama wa chuma wa Liganga na makaa ya mawe
wa Mchuchuma ameanza kuisikia muda mrefu, lakini hajaona utekelezaji.
Bashe alisema Waziri Dk Mpango anazungumzia bajeti ya Sh33 trilioni na
kwamba eneo la kwanza ni makusanyo ya kodi kuongezeka kwa asilimia 16,
wakati siyo mazuri.
Alisema wabunge waliwahi kuwaambia wasiweke kodi
kwenye uhamishaji wa fedha, utalii na maeneo mengine, lakini
hawakuwasikia.
Ndalichako
Wakizungumzia hali ya elimu, wabunge
walimkosoa Waziri Ndalichako kutokana na hali inavyoendelea, hasa suala
la mikopo ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.
Akichangia eneo hilo,
Heche alianza kwa kukosoa kitendo cha Profesa Ndalichako kwenda kupiga
kura katika uchaguzi wa meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni
uliofanyika wiki mbili zilizopita jijini Dar es Salaam.
“Leo elimu ni
majanga. Mimi nilikuwa nakuheshimu sana Profesa Ndalichako ukiwa Katibu
wa Baraza (la Mitihani la TaifaNecta). Umewahi kuonyesha watu wamechora
mazombi kwenye mitihani,” alisema.
“Wewe umepewa wizara hii, umechora
Zombie kubwa kuliko wale waliochora kwenye mitihani, sijui hata wizi wa
mitihani utazuiaje kama wewe Profesa ulitoka hapa kwenda kuiba kura
Kinondoni.”
Alisema hivi sasa Bunge wamelifanya kama idara fulani ya
Ikulu inayohusika na umwagiliaji maji katika maua.
Mbunge wa Ukonga
(Chadema), Mwita Wataira alisema Ndalichako alipiga kura za kuwachagua mameya wa halmashauri za manispaa za
Kinondoni na Ilala.
“Ulikuwapo juzi kwenye uchaguzi wa meya Kinondoni
wakati ulishapiga kura katika umeya wa Ilala, Profesa mzima unahusika
katika wizi wa kura,” alisema.
Mwijage
Pia Waziri Mwijage alikuwa kwe-
nye kikaangio hicho. Akichangia suala la mpango wa Serikali kuifanya
Tanzania iwe nchi ya viwanda, Dk Chegeni alisema Mwijage ni “mzee wa
sound” ambaye anafanya porojo.
“Waziri wetu anajulikana kama mzee
wa porojo, sijui hiyo
Tanzania ya viwanda tutafika lini. Acheni maneno maneno na kusigana
wenyewe kwa wenyewe. Mnatofautiana kauli, kila mmoja anaongea lake.
Fanyeni kazi kwa pamoja kila wizara itoe maoni yake katika huo Mpango,”
alisema Dk Chegeni.
Naye
Heche alisema hata kwa Watanzania wanamjua
Mwijage kwa jina la “Mzee wa Sound”. “Ukikutana naye hapo nje
ukamsimamisha waziri, anauliza ‘vipi unataka nikupe kiwanda’ na kutoa
mkono
mfukoni.
Anataka kuchomoa kiwanda mfukoni? Mpango wenu hamjajenga
kiwanda hata kimoja,” alisema.
Alisema kiwanda ndicho kitaajiri watu
wengi wakiwemo mamantilie, wahasibu wahandisi na wengine wengi, lakini
hadi sasa hakuna kiwanda hata kimoja.
Kairuki
Akizungumzia suala la
watumishi hewa, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo) Zitto Kabwe
alionyesha kushangazwa na kitendo cha mawaziri kutoa taarifa
zinazotofautiana.
“Monthly Economic Review (taarifa ya uchumi ya mwezi)
ya Agosti 2015 inaonyesha kwamba wages and salaries (mishahara) ambazo
Serikali ililipa Juni mwaka 2015 zilikuwa Sh456 bilioni.
"Monthly
Economic Review ya Agosti 2016 inaonyesha kwamba wages and salaries
ambazo Serikali imelipa kwa mwezi Juni 2016 ni Sh534 bilioni,” alisema
Zitto.
“Kwamba kuna nyongeza ya gharama za mishahara ya kila mwezi ya
Sh78 bilioni. Waziri wa Utumishi jana ameeleza wanaokoa Sh19 bilioni
kila mwezi kwa kuondoa watumishi hewa. Taarifa ya Benki Kuu inaonyesha
kuwa tangu Serikali hii iingie madarakani, gharama za watumishi kwa mwezi
zimeongezeka kwa Sh78 bilioni.”
Zito alisema pamoja na watumishi hewa
kuondolewa, ajira mpya kuzuiwa na nyongeza ya mishahara kusimamishwa,
gharama za mishahara zimeongezeka kwa Sh78 bilioni. “Haiekeweki.
Kuna
mmojawapo kati ya hawa wawili (Waziri Kairuki na BOT) anadanganya umma.
Ama zoezi la watumishi hewa ni publicity stunt (la kujitafutia umaarufu)
au Serikali inatumia fedha kwa matumizi mengine, halafu BOT inasema ni
mishahara,”alisema Zitto.
Post a Comment