0
Naibu Waziri wa Elimu, Philipo Mulogo
Naibu Waziri wa Elimu, Philipo Mulogo
WANAFUZI watatu wa Shule ya Msingi Ussongo, kata ya Nyandekwa, wilayani Igunga mkoani Tabora, wamepatiwa ujauzito. Wanamtuhumu mwalimu wao, Baraka Samsoni.
Wanafunzi wanaodai wamepewa ujauzito na Mwalimu Samsoni, ni  Christina Gordwin (15), Magdalena Bakari (15) na Lusia Maganga (17). Wote watatu wanasoma darasa la saba shuleni hapo.
Wakizungumza na waandishi wa habari, Christina ambaye hakuweza kufanya mtihani wake wa kuhitimu elimu ya msingi, alidai kuwa  mahusiano ya kimapenzi na mwalimu wake yalianza tangu Januari mwaka huu.
Naye Christina Mhindi (70) bibi wa Christina Gordwin amesema, siku ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi alimpeleka mjukuu wake shuleni na kuomba aruhusiwe kufanya mtihani lakini alikataliwa kutokana na kuwa na ajauzito huo.
“Mjukuu wangu ameshindwa kufanya mtihani wake wa mwisho kwa sababu ya ujauzito. Haingii akilini kuona walimu tuliowamini kufundisha watoto wetu, ndiyo hao hao wanaowaharibu. Kinachoniuma zaidi, ni kuona hakuna hatua zinazochukuliwa,”ameeleza.
Akiongea kwa uchungu huku chozi likimminika, Bi. Mhindi amesema, “Kinachoniuma zaidi, mjukuu wangu anazuiwa kufanya mtihani, wakati wenzake wawili waliopewa ujauzito na mwalimu huyo huyo, wameruhusiwa kufanya mitihani yao.”
Falentina Lugamba, mwalimu mkuu wa shule hiyo, amekiri wanafunzi hao kupata ujauzito.
“Haya madai yapo ofisini kwangu. Nimeambiwa kuwa mwalimu Baraka ndiye aliyewapa wanafuzi hawa ujauzito,” amesema Mwalimu Lugamba katika mahojiano na MwanaHALISI online wiki hii.
Amesema kwa sasa mwalimu anayetuhumiwa kuwapa mimba wanafuzi wake,  hayuko kazini na kuongeza, “Tayari nimetoa taarifa kwa ofisi wa elimu wilaya kuhusu utoro wa mwalimu huyo.”
Kaimu ofisa Mtendaji wa kata ya Nyandekwa, Jaquiline Gube, amekiri kupokea taarifa hizo kwa mmoja wa  wazazi wa  wanafunzi. Alisema mzazi huyo ameomba kushughulikiwa; tayari amemwandikia mkuu wa shule na mtendaji wa kijiji hicho kufuatilia suala hilo.

Post a Comment

 
Top