0

TUNDU Lissu, Mwanasheria Mkuu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameiangusha Jamhuri katika kesi ya kumkashifu JPM iliyokuwa ikimuhusu Dennis Wilson

Wilson, mwanachama wa Chadema alishtakiwa na Jamhuri ya Tanzania katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kwa kuandika maneno ya kuudhi na kutaja jina la JPM katika mtandao wa kijamii.

Katika taarifa zilizotufikia muda huu kutoka Kisutu zinaeleza kuwa, mahakama hiyo imetupilia mbali kesi hiyo kutokana na washitaki (Jamhuri) kushindwa kufafanua uhalisi wa kifupisho JPM.

“Sababu ni hati magumashi ya mashtaka ambayo haikuwa na maelezo ya kutosheleza kwasababu watesi wetu (Jamhuri) hawakufafanua maana ya kifupisho ‘JPM’ ambaye ndiye walidai ameudhika na maneno ya Wilson.

“Mahakama imekubaliana na hoja yetu kwamba, JPM inaweza kuwa kifupisho cha Juma Pumba Maharage au majina yoyote yanayoanzia na JPM.

“Mahakama imewaelekeza washtaki kama wanataka kuendeleza vita yao basi walete hati ya mashtaka inayoeleweka,” amesema Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki.

Hata hivyo, baada ya mahakama kutupilia mbali shauri la Jamhuri, mshtakiwa (Wilson) alikamatwa tena.

“Tunawasubiria warudi tena mahakamani. Wakirudi tutaomba huyo JPM aliyeudhika na maneno ya Wilson aje atoe ushahidi wa kipi kilichomuudhi,” amesema Lissu

Post a Comment

 
Top