0
Mchakato wa kumpata mgombea urais umeendelea kukichanganya Chama cha ACT – Wazalendo na sasa kimelazimika kuanza upya vikao vya kumpata mgombea mwingine atakayepeperusha bendera ya urais kwa tiketi ya chama hicho.
Mkanganyiko huo umetokea baada ya mgombea aliyeteuliwa   na kuchukuliwa fomu na chama hicho ya kugombea nafasi hiyo, Profesa Kitila Mkumbo kukataa uteuzi huo juzi, huku zikiwa huku zikiwa zimebaki siku mbili kumalizika kwa mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu. Katibu wa Mipango na Mikakati wa ACT – Wazalendo, Habibu Mchange aliwaambiwa waandishi wa habari jana kuwa chama hicho kinaanza leo mchakato wa kumpata mgombea atakayebeba jukumu hilo baada ya Profesa Mkumbo kukataa uteuzi wa chama.
Alisema mchakato huo utaanza na mkutano wa Kamati Kuu utakaofanyika leo na kufuatiwa na mkutano wa Halmashauri Kuu utakaofanyika kesho, kisha mkutano wa kidemokrasia kwa ajili ya kutafuta mbadala wa Profesa Mkumbo. “Baada ya vikao hivyo ndipo tutamtaja rasmi mgombea wetu na zoezi la kutafuta wadhamini litaanza siku hiyohiyo,” alisema Mchange. Mchange alisema tayari wagombea watatu wameshajitokeza kuwania nafasi hiyo.
“Tuna wagombea watatu tena wenye sifa, wameshachukua fomu za kuwania nafasi hiyo, kwa hiyo kazi ya vikao ni kuangalia yupi anafaa zaidi kati yao na ndiye atakayechaguliwa,” alisema Mchange ambaye alikataa kutaja majina hayo. Wakati ikiwa inaonekana kwamba chama hicho kitalazimika  kukimbizana na muda ili kukamilisha mambo hayo ndani ya muda uliopangwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kiongozi huyo alisema wameshasambaza fomu za wadhamini hivyo muda uliyobaki unatosha. “Fomu zimeshasambazwa mikoani kwa hiyo tukimpata mgombea zitajazwa na kurejeshwa ndani ya muda na  tutarudisha fomu NEC kama utaratibu unavyotaka,” aliongeza, Katibu wa Fedha na Rasilimali wa chama hicho, Peter Mwambuja.
Kuhusu mgombea mwenza aliyetajwa juzi kuwa ni kada wa chama hicho kwa muda mrefu, Hawra Shamte, kiongozi huyo alifafanua kuwa baada ya mgombea urais kutangazwa naye atatambulishwa rasmi. Hata hivyo alisema jina hilo halihusiani na Hawra Shamte ambaye ni mmoja wa wahariri wa gazeti la Mwananchi, jambo ambalo hata Shamte mwenyewe alilikanusha juzi.

Post a Comment

 
Top