0
Sumbawanga. Mgombea wa urais kupitia CCM, Dk John Magufuli ameendelea kumwaga ahadi mikoa ya Katavi na Rukwa na kuahidi kuwa iwapo atachaguliwa kuwa rais wahudumu wanaoiba dawa katika hospitali nchini watakiona cha moto.

Akiwahutubia wakazi wa Namanyere mkoani hapa leo, Dk Magufuli alisema anataka kutengeneza nchi isiyo na kero ikiwemo kuondoa tatizo la uhaba wa dawa.

Mgombea huyo,  ambaye jana aliingia siku ya pili kuzunguka mikoani kuomba kura,  alisema tabia ya watu kwenda hospitali kutibiwa na kuambiwa wakanunue dawa  kwenye maduka kwa kuwa vituo vya afya havina dawa,   ataikomesha.

"Nafahamu kuna matatizo ya dawa kwenye hospitali eti ukienda kutibiwa unaandikiwa cheti ukanunue dawa mahali pale, sasa pale wamepataje hizo dawa?" alihoji.

"Wale wote wenye tabia ya kuiba kuiba dawa, madaktari, ili wapeleke sehemu nyingine, moto wao unakuja."

Alisema akingia madarakani atahakikisha dawa zinapatikana  kila hospitali na ili kutatua tatizo la wizi wa dawa ataboresha masilahi ya madaktari na manesi.

Dk Magufuli ambaye muda wote amekuwa akiwataka wananchi wamwamini kwa ahadi zake, alisema siku zote anachukia rushwa, uzembe, na manyanyaso kwa wengine huku baadhi wakifaidi rasilimali za nchi.

Post a Comment

 
Top