0
Hamfrey Polepole na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa wamekabana kwa hoja kali kuhusu uamuzi wa Chadema na Ukawa kwa ujumla kumpokea Edward Lowassa na kumpa nafasi ya kugombea Urais.Polepole na Msigwa walikutana jana katika kipindi cha ‘Mada Moto’ kinachorushwa na kituo cha runinga cha Chanel Ten kujadili mada iliyotajwa kama ‘Lowassa Ndani ya CCM’.Polepole alionesha msimamo wake wa kumkataa Edward Lowassa kuwa sio kiongozi sahihi aliyepaswa kuungana na Ukawa katika safari yao ya kutaka kuongoza dola na kupata katiba mpya ya wananchi kwa kuwa ana tuhuma nzito zilizompa madoa.Aliongeza kuwa dhana ya upinzani na mwenendo wa Ukawa ulipotea pale walipomkaribisha Lowassa huku wakisahau kuwa ni miaka michache iliyopita walizunguka nchi nzima kuwaaminisha watanzania kuwa ni fisadina kwamba wana ushahidi wa kutosha.Polepole ambaye alikuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iyoongozwa na Jaji Warioba, alisema kuwa Ukawa iliundwa kwa madhumuni ya kutetea Katiba ya Wananchi na sio kwa lengo la kisiasa kama ilivyo sasa.Alisema kuwa Edward Lowassa hana msimamo thabiti kwenye maamuzi yake kuhusu Katiba anayoitaka kwa kuwa aliwahi kumhoji awali akasema anahitaji muundo wa serikali tatu lakini baadae alimfuata na kumueleza kuwa amebadili anataka muundo wa serikali mbili.“Lowassa niliongea naye wakati huo nakusanya maoni kuhusu katiba mpya, mara ya kwanza alisema anataka serikali tatu na akaandika kwenye kumbukumbu maalum za bunge. Lakini baadae alinifuata tena na kubadili msimamo wake akitaka serikali mbili,” alisema Polepole.Anasema kilichomshangaza zaidi kwa Lowassa ni pale alipopendekeza kuwa anataka muundo wa serikali mbili na kwamba serikali hizi mbili ziwe na uhusiano wa kijeshi pekee.Akiendelea kutetea hoja yake ya kumpinga Lowassa, PolePole alisema kuwa amewahi kufanya kazi na Lowassa na kwa undani kabisa aligundua kuwa ni mbinafsi.“Watanzania mnatakiwa kufahamu kuwa mnapokutana na Lowassa, Ninyi sio kitu bali kitu ni Lowassa,” alisema.Mjadala huo ulitawaliwa na mivutano binafsi iliyowalazimisha kutoka nje ya mada mara kadhaa hususan baada ya Mchungaji Msigwa kutoa tuhuma za Polepole hadharani kisha akampa nafasi ya kujitetea.Baada ya PolePole Kujitetea kufuatia tuhuma hizo, Mchungaji Msigwa alimueleza kuwa alichokifanya ndio kinaitwa ‘natural justice’ ambayo Edward Lowassa hakupewa wakati ule.Akizijibu hoja za Polepole huku kukiwa na majibishano ya hapa na pale, Mchungaji Msigwa alikiri kuwa yeye ni mmoja kati ya wanachama wa Ukawa waliomsema sana Edward Lowassa na kumuita fisadi lakini sasa ameamua kukaa kimya.“It’s true tulisema. Hata mimi nilisema, it’s true I can’t deny it. Lakini hata Joe Biden (Makomo wa pili wa Marekani) alikuwa anamsema Obama kuwa ‘he does not fit for Commander in Chief, lakini alipochaguliwa wakafanya kazi pamoja. Hatuwezi kusema kana kwamba Lowassa ndiye muovu kuliko mtanzania yeyote hapa nchini,” alisema.Aliongeza kuwa kitu kikubwa alichojifunza kwa Lowassa na kumfanya amheshimu sana, ni moyo wa uvumilivu na kukaa kimya hata pale alipokuwa akitukanwa kila kona na kuitwa Fisadi. Alisema moyo huo wa uvumilivu hata watumishi wengi wa Mungu hawana.Alifafanua kuwa katika ulimwengu wa siasa ni kawaida kufanya kazi na mwanasiasa ambaye awali ulikuwa ukimpinga sana kwa kuwa muda ukifika akaamua kubadilika mambo hubadilika pia.Msigwa alisema kuwa chama chao ni chama cha demokrasia na maendeleo na kwamba hilo ndilo limewapelekea kumfungulia mlango Edward Lowassa baada ya kumhoji na kumuelewa.Alipinga hoja ya Polepole kuwa Lowassa ana mapesa mengi ambayo ameyapata kwa njia zisizofahamika, Msingwa alisema kuwa maelezo hayo hutolewa bila kuelezewa kwa undani kama ana pesa nyingi kuliko nani (serikalini).“Unasema Lowassa ana mapesa mengi, ni kama vile unajua akaunti zote za Lowassa zina shilingi ngapi. Na husema ana fedha nyingi kuliko nani?”Aliwataka watanzania kutomchukulia Lowassa kama vile ndiye mtanzania mwenye dhambi nyingi kuliko wote bali wajikite katika kuangalia nia yake ya dhati ya kuleta mabadiliko ya kweli nchini.Alisisitiza kuwa Chadema hawana muda wa kumsafisha Lowassa kwa kuwa umati uliofurika kumsindikiza kuchukua fomu ya kugombea urais katika ofisi za Tume ya Uchaguzi Mkuu (NEC) inaonesha jinsi ambavyo watanzania wana Imani naye.Alisema kuwa kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika hivi karibuni zinaonesha kuwa ni asilimia 5 hadi 8 tu ya watanzania ambao wamejikita katika kufahamu ufisadi wa wagombea na kwamba umma mkubwa unataka mabadiliko kwa kuwa wamechoshwa na muundo.Msigwa alimtaka PolePole kutomzungumzia Lowassa pekee kwa mtazamo hasi bali azungumzie pia ubaya wa Magufuli ambaye anaunga mkono muundo wa serikali mbili kinyume na ile anayoisapoti Polepole na Tume Ya Mabadiliko Ya Katiba. Na kwamba yapo maovu mengi kwenye wizara ya ujenzi inayoongozwa na Mafuli.Akijibu hoja ya Msigwa, PolePole alisema kuwa yeye ni mmoja kati ya watu walioishawishi CCM kukata majina ya wagombea wote wenye madoa katika mchakato wa kura za maoni kumpata mgombea urais.Alisisitiza kuwa ingawa CCM ni chama chake, hatampigia kampeni Magufuli hadi pale ambapo rufaa zilizokatwa dhidi ya wagombea waliotangazwa kuwa washindi wa kura za maoni ziangaliwe na wote wenye madoa waondolewe.
“Ili niwaunge mkono, CCM mnatakiwa kuwakata watu wote katika mchakato wa kura za maoni wanaotuhumiwa kwa kashfa mbalimbali,” alisema Polepole ambaye awali alitangaza kutembea nchi nzima kuhamasisha watu wasimchague Lowassa.PolePole alitoa ushauri pia kwa chama chake cha CCM ili kiwe tofauti na makosa yaliyofanywa na wahasimu wao wa kisiasa, Ukawa.“Viongozi wa CCM, kama Ukawa wamewachukua watuhumiwa wamewakubali. Nyie onesheni uongozi na utofauti mhakikishe mnawakata wagombea wote wanaotuhumiwa. Onesheni kwamba watuhumiwa hawana nafasi kwenu.

Post a Comment

 
Top