0
Sasa ni rasmi; Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Pombe Magufuli watavaana katika mpambano wa kuwania kuingia Ikulu, baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwapitisha kugombea urais pamoja na wengine sita, huku watatu wakitemwa.
Wakati Lowassa atagombea urais kwa tiketi ya Chadema, akiungwa mkono na vyama vinne vinavyounda Ukawa, Dk Magufuli anawania nafasi hiyo kwa tiketi ya CCM, huku mwanasiasa maarufu nchini, Mchungaji Christopher Mtikila akikataliwa kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho pamoja na wengine wawili.
Wawili hao na wengine sita walipitishwa jana na NEC ikiwa ni siku ya mwisho kwa wagombea kurejesha fomu kwenye ofisi za Tume, huku wagombea ubunge na udiwani wakirejesha wilayani.
Wagombea wengine waliopitishwa kuwania urais na wako huru kuanza kampeni leo ni Fahmy Dovutwa wa UPDP, Maxmilian Lyimo (TLP), Chifu Lutalosa Yemba (ADC), Anna Mghwira (ACT-Wazalendo), Janken Kasambala (NRA) na Hashim Rungwe (Chaumma).
Mchungaji Mtikila pamoja na Lifa Chipaka wa Tadea na Dk Geofrey Malisa (CCK) wameondolewa kwenye orodha ya wagombea urais.
Pamoja na mbio za urais kujumuisha wagombea nane, mpambano mkali unatarajiwa kuwa kati ya Lowassa, ambaye ameongeza nguvu ya upinzani kutokana na umaarufu wake na muungano wa vyama vinne vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD, na Dk Magufuli, ambaye anawakilisha chama chenye mtandao mkubwa nchini.
Wote wawili wamefikia hatua hiyo ya kuomba kura za wananchi kwa mara ya kwanza, lakini Lowassa alijaribu kugombea kwa mara ya kwanza mwaka 1995 na jina lake likakatwa na Kamati Kuu, kama ilivyokuwa mwaka huu.
Mwaka huu aliamua kutokata tamaa na akajiunga na Chadema, ambayo imempa fursa ya kugombea urais.
Jana kwenye ofisi za NEC, mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume hiyo, Kailima Kombwey alisema Mchungaji Mtikila amepoteza sifa kutokana na kutokuwa na mgombea mwenza, kutokula kiapo Mahakama Kuu, kutokamilisha mahitaji ya fomu namba 8A, kutolipa dhamana ya Sh1milioni na kuchelewa kufika NEC kabla ya saa 9:30 alasiri, muda uliokuwa wa mwisho kwa wagombea kurejesha fomu.
Lakini Mchungaji Mtikila, ambaye amekuwa akieleza wazi kuwa anapinga Muungano, alisema mgombea mwenza, ambaye alitakiwa kutoka Zanzibar, aliuguliwa na mkewe.
“Nimeshindwa kuja na mgombea mwenza kwa sababu mke wake ameugua presha ghafla. Jambo hilo lilimfanya ashindwe kufika hapa,” alisema.
Mtikila alidai kuwa alifika mapema NEC, lakini alilazimika kwenda Mahakama Kuu kwa ajili ya kuapa. Alidai kuwa mahakamani alitumia zaidi ya saa mbili kumsubiri mgombea mwenza, Juma Metu Juma ambaye hakutokea.
“Nilipotaka kumuona mkurugenzi (Kombwey) nilijibiwa kuwa anashughulikia tatizo langu. Lengo lilikuwa kutaka kumueleza tatizo nililonalo. Kwanza taratibu na kanuni za NEC hazisemi chochote iwapo mgombea mwenza anapata dharura,” alisema Mtikila ambaye alikiri kuwa hakulipa Sh1milioni licha ya kuwa nayo mfukoni.
Baada ya maelezo yake kutoishawishi NEC, Mchungaji Mtikila alisema: “Mimi kugombea si tatizo, ila nataka kuweka mambo sawa. Hata nisipogombea hiyo hainizuii kwenda mbinguni. Kwanza mtu mwenye uchu wa madaraka ya kwenda Ikulu anatakiwa kuepukwa kama ukoma.”
Mwaka 2010, Mtikila pia alishindwa kutekeleza masharti na hivyo kupoteza sifa za kuteuliwa na NEC kugombea urais sambamba na Mwenyekiti wa Chama cha Sauti ya Umma (Sau), Paul Kyara.
Mgombea mwingine aliyeondolewa ni Chipaka wa Tadea, ambaye alifika NEC bila ya mgombea mwenza na hivyo kutotimiza masharti.
“Tadea wameshindwa kukidhi vigezo vilivyopo katika fomu namba 8A hivyo hawana sifa,” alisema Kombwey.
Chipaka, ambaye kama Mtikila naye alitumia usafiri wa bajaji, hakuwa na maelezo ya kujitetea alipotakiwa kufanya hivyo, akisema hakuwa na cha kuzungumza.
Alisema mgombea wa AFP, Omar Mohamed Sombi, hakutokea kabisa licha ya chama hicho kuthibitisha kusimamisha mgombea urais na kuingizwa katika ratiba.
Dk Malisa wa  CCK alisema ameshindwa kutimiza  masharti kwa sababu ya kesi aliyoifungua Makakama Kuu.
Alisema walifungua kesi kupinga urasimu uliopo wakati wa kutafuta wadhamini baada ya baadhi ya vitambulisho vya taifa kutotambulika kwa wakurugenzi wa wilaya.
Alisema Mahakama Kuu iliona haja ya kulipitia suala hili kwa sababu siyo kazi yao kuangalia vitambulisho bandia au halali hiyo ni kazi ya Tume.
“Tumemshitaki mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva, kwa sababu yeye ndiyo ametajwa kila mahali katika Sheria za Tume na ndiyo ameteuliwa na rais, pamoja na jaji Mkuu kwa sababu ndiyo Mwanasheria Mkuu wa nchi wakati vitu vya kihuni kama hivyo vinafanyika,” alisema Dk Malisa.
Dk Malisa pia alilalamikia muda wa kutafuta wadhamini wa siku 21 kuwa ni mdogo huku akilalamikia rushwa, akisema kila waliyemfuata alikuwa anaomba apewe fedha.
“Hatuishii hapa kama mahakama haikutoa haki tutakwenda mbele. Kama (Baba wa Taifa) Mwalimu Julius Nyerere alikwenda hadi Umoja wa Mataifa kudai haki, na sisi tutafanya hivyo ingawa bado tuna imani na mahakama, ”alisema.
Wagombea wote wa urais walitakiwa kutumiza masharti manane yaliyopo katika fomu namba 8A ambayo ni kutoa taarifa za maelezo binafsi ya mgombea urais na mgombea mwenza, tamko la mgombea urais na mgombea mwenza, tamko la kisheria lililotiwa muhuri wa Mahakama Kuu.
Masharti mengine ni majina 200 ya wadhamini wa mikoa 10 ya Tanzania Bara na visiwani, uthibitisho wa chama cha siasa kumdhamini mgombea, uthibitisho wa msimamizi wa uchaguzi, mgombea kuweka dhamana ya Sh1milioni na tamko namba 10 la kuheshimu na kutekeleza maadili ya uchaguzi.
Ilivyokuwa
Wa kwanza kufika NEC alikuwa mgombea Lowassa, ambaye alitinga ofisi hizo saa 3:42 asubuhi akiongozana na mkewe, Regina na mgombea mwenza, Juma Duni Haji na Makamu wa kwanza wa rais Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad.
Baadaye alifika mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na wa Freeman Mbowe (Chadema) na makada wa zamani wa CCM, Goodluck Ole Medeye na Hamis Mgeja.
Kwa mujibu wa ratiba na NEC, Lowassa alitakiwa kuchukua fomu saa 4:00 asubuhi na kufuatiwa na mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli saa 5:00 asubuhi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Lowassa alisema ametimiza masharti yote ya NEC, huku Mbowe akisema Ukawa itatoa ratiba ya kampeni kwa vyombo vyote vya habari.
Kwa upande wake Dk Magufuli, aliyekuwa amevaa shati la kijani na suruali nyeusi akiambatana na Samia Suluhu, ambaye ni mgombea mwenza, Ramadhan Madabida (mwenyekiti wa CCM wa Dar es Salaam), Abdallah Bulembo (mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM), Phillip Mangula (makamu mwenyekiti-Bara), na Rajab Luhavi (naibu katibu mkuu) na Zakhia Meghi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilisha taratibu zote, Dk Magufuli alisema alienda NEC kutimiza masharti kama alivyoagizwa huku akiwaonyesha waandishi wa habari fomu yake ya uteuzi.
“Mimi na mwenzangu ni watu wa kutii sheria na leo (jana) tumefanya hivi  kama mnavyotuona hapa,” alisema Dk Magufuli ambaye wakati wa kushuka kutoka ofisi ya NEC zilizopo ghorofa ya saba alitumia ngazi badala ya kupanda lifti .
Wakati akiondoka saa 5:25 aliawaaga waandishi wa habari huku akirudia msemo wake wa kuwataka Watanzania wamuombee, na kupiga picha pamoja na baadhi ya wanahabari.
Dk Magufuli alifuatiwa na mgombea urais wa TLP, Macmillan  Lyimo ambaye baada ya kumaliza taratibu zote aliwaeleza waandishi wa habari kuwa chama hicho kitazindua kampeni zake mkoani Kilimanjaro kwa maelezo kuwa jijini Dar es Salaam kuna msongamano.
Saa 6:20 mchana alifika mgombea urais wa ADC,  Chief Lutalosa Yemba akiwa ameongozana na wanachama wasiozidi kumi akiwamo mgombea mwenza na mwenyekiti wa chama hicho, Said Miraj.
Baada ya kutimiza masharti yote, Yemba alisema lengo lake ni kuongoza badala ya kutawala kama wanavyofanya viongozi wengi waliopo madarakani hivi sasa.
Kuhusu gharama za uchaguzi, alisema hilo si tatizo kwake kwa maelezo kuwa chama hicho kimesaidiwa na wananchi wenye mapenzi mema.
“Tutaanzia kampeni zetu Tanga, Agosti 30. Tunaomba Watanzania watukubali, watupe nchi tuwaonyeshe mema ya nchi hii,” alisema Yemba.
Mghwira, mgombea urais wa ACT-Wazalendo ambaye alipitishwa juzi usiku na Halmashauri Kuu, alifika ofisi za NEC saa 7:35 mchana na baada ya kukamilisha taratibu zote, alisema chama hicho kilitumia mtandao kupata wadhamini kama ilivyotakiwa na Tume ya Uchaguzi.
Kasambala, ambaye anaiwakilisha NRA, alisema kuwa amejipanga hasa kuangalia masuala muhimu kama ya watoto na akina mama.
Alisema yeye ni askari mstaafu na anajua jinsi wastaafu wenzake wanavyopata shida, hivyo atawasaidia.
“Sikutaka kugombea, nilisikiliza watu gani wanaochukua fomu kugombea nilipowatambua sikuona suluhisho la Watanzania. Nikachukua fomu ili kuwapatia suluhisho,”alisema Kasambala.
Alieleza kuwa chama chake kitaanza kampeni Agosti 29, mkoani Kigoma, akisema mpango wake ni kuanzia mpakani na kurudi maeneo mengine ya nchi.
Mgombea mwingine, Rungwe aliingia ofisi za Nec akiwa ameongozana na mgomea mwenza, Issa Abbas, na wafuasi wasiozidi sita.
Baada ya kurudisha fomu Rungwe alisema kuwa hatishwi na mtu kwa kuwa hajaona wa kumtisha miongoni mwa wagombea urais, hivyo lengo lake la kuwasaidia Watanzania lipo pale pale na anaamini atafanikiwa. Alisema hatishwi na wagombea wanaokuwa na kundi kubwa la wafuasi kwa sababu alipokuja Papa John Paulo ll , watu walijazana Jangwani, lakini wote hawakuwa Wakristo.
“Nitapambana nikiwa na nia moja ya kushinda na kuwasaidia Watanzania. Kampeni nitaanzia Tandale shule leo kumtambulisha mgombea ubunge kwa tiketi ya Chaumma wa Jimbo la Kinondoni,” alisema Rungwe.
Imeandaliwa na Fidelis Butahe, Kalunde Jamal na Bakari Kiango
StarTV 

Post a Comment

 
Top