AZAM FC ina kibarua kigumu cha kufuta uteja kwa Yanga katika mechi za Ngao ya Jamii wakati zitakapomenyana leo katika mechi ya kufungua msimu wa 2015-16 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo itakuwa ya tatu mfululizo kwa timu hizo mbili ambazo zimekuwa na ushindani mkubwa katika soka la Tanzania baada ya kudorora kwa Simba katika miaka ya karibuni hasa katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Tangu msimu wa 2012-13, Yanga na Azam FC zimekuwa zikipokezana katika nafasi mbili za kwanza za ubingwa wa Bara, Yanga ikitwaa taji msimu uliomalizika baada ya klabu ya Chamazi kutawazwa kwa mara ya kwanza msimu wa 2013-14 ikilipoka taji kutoka kwa vijana hao wa Jangwani.
Lakini katika mechi za Ngao ya Jamii ambazo hukutanisha bingwa na mshindi wa pili, mara mbili mfululizo Yanga imeibuka mshindi ikianza kwa ushindi wa bao 1-0 la Salum Telela kabla ya Agosti mwaka jana kushinda kwa mabao 3-0, yakifungwa na Geilson Santana Santos maarufu Jaja na Simon Msuva.
Hivyo, Azam FC leo itakuwa na kibarua kikali cha kubadili matokeo hayo mbele ya mashabiki kwenye uwanja huo mkuu wa Taifa, ingawa timu hiyo imekuwa ikipata ushindi katika Ligi Kuu dhidi ya Yanga.
Katika msimu uliomalizika, mechi ya kwanza ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2 kabla ya Azam FC kushinda mabao 2-1 na kupata nafasi ya pili katika ligi na kuipiku Simba iliyokuwa ikinyemelea nafasi hiyo.
Aidha, katika michuano ya Kombe la Kagame iliyomalizika mapema mwezi huu kwenye Uwanja wa Taifa, Azam iliishinda Yanga kwa penalti katika mechi ya robo fainali baada ya sare ya 0-0 katika dakika 90 na kikosi hicho cha Mwingereza Stewart Hall kwenda hadi nafasi na kutwaa ubingwa ikiizamisha Gor Mahia kwa mabao 2-0.
Kwa hiyo, mechi ya leo inatarajiwa kuwa ya ushindani mkubwa kutokana na matokeo hayo ya nyuma, lakini pia kwa sababu ya uimara wa usajili wa timu hizi mbili ambazo kwa sasa zimelikamata soka la Tanzania, si tu kwa ubora wao uwanjani, bali hata kwa uwezo wao wa kifedha.
Azam FC inajivunia fedha za mmiliki wake, mfanyabiashara maarufu na tajiri nchini, Said Salim Bakhresa wa makampuni ya Bakhresa Group wakati Yanga inaongozwa na Mwenyekiti ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu na tajiri nchini, Yusuf Manji ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Quality Group.
Fedha za matajiri hao wawili zimewezesha timu hizo kusajili wachezaji wanaowataka ndani na nje ya nchi na hilo linathibitishwa na kuwapo kwa wachezaji saba wa kigeni katika Yanga ambao ni Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite, Amissi Tambwe, Andrey Coutinho, Donald Ngoma, Thabani Kamusoko na Vincent Bossou.
Kamusoko na Bossou wamesajiliwa mara tu baada ya kumalizika kwa Kombe la Kagame, huku Kamusoko ambaye ni kiungo akitokea FC Platinum ya Zimbabwe na beki wa kati kutoka Togo, Bossou alikuwa akicheza barani Asia.
Kwa Azam, inao nyota wa kigeni kama Michael Balou, Kipre Tchetche, Didier Kavumbagu, Jean Mugiraneza, Pascal Wawa na Alan Wanga ambaye ni Mkenya, hajaanza kucheza kutokana na kufiwa na mama yake.
Aidha, vikosi vyao vinajivunia wachezaji wa ndani wanaotesa kwa sasa kama Geoffrey Mwashiuya, Deus Kaseke, Haji Mwinyi, Malimi Busungu na Mateo Simon ambao ni wapya kwa upande wa Yanga, lakini tayari baadh yao wameanza kuonesha cheche zao.
Simon amesajiliwa kutoka KMKM baada ya Kombe la Kagame. Ame Ali na Ramadhani Singano ni wapya katika kikosi cha Azam lakini makali yao yanafahamika kwa wapenzi wa soka nchini ambao watafurika kwa wingi leo kupata uhondo wakati wakijiandaa na Ligi Kuu ya Bara inayoanza Septemba 12, mwaka huu, wiki moja baada ya Taifa Stars kucheza na Nigeria ‘Super Eagles.’
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), mechi hiyo itaanza saa 10 kamili jioni na itachezeshwa na mwamuzi kutoka Morogoro, Martin Saanya badala ya Israel Nkongo wa Dar es Salaam ambaye ni mgonjwa.
Ilisema tiketi zitaanza kuuzwa leo asubuhi katika magari maalumu maeneo ya Uwanja wa Taifa ambako kiingilio cha chini kitakuwa Sh 7,000 na kiingilio cha juu ni Sh 30,000 kwa VIP A.
Kabla ya mchezo huo, kutakuwa na mchezo wa utangulizi utakaozikutanisha timu ya wachezaji wa zamani wa timu ya Taifa (Taifa Stars Legends) dhidi ya Ukonga Veterani, ilisema TFF na kuongeza kuwa milango ya uwanja itakuwa wazi kuanzia saa tano kamili asubuhi.
Post a Comment