Waislamu wote nchini wametakiwa kuadhimisha Siku ya Maulid kwa kufanya usafi, kupanda miti na kuchangia damu.
Aidha, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Siku ya Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W).
Hata hivyo, ugeni rasmi wa Waziri Mkuu Majaliwa unategemea ratiba yake.
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Mufti wa Tanzania, Shehe Abubakar Zubeir wakati akizungumzia Siku ya Maulid ambayo alisema kwa mwaka huu, Maulid itasomwa usiku wa Desemba 11, na kitaifa itafanyika Kata ya Shelui wilayani Iramba Mkoa wa Singida na mapumziko yatakuwa siku inayofuata yaani Desemba 12.
Mufti Zubeir alisema Waislamu wanatakiwa kutumia siku hiyo kuonesha matendo mema na yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu pamoja na kuisaidia jamii kufanya usafi kwenye mitaa yao na kuchangia damu ili kusaidia wenye uhitaji huo.
Alisema anatakiwa kiongozi kufanya matendo hayo wanapoifurahia siku ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) ambaye amesema uislamu ni usafi, basi jisafisheni wenyewe.
“Mimi na familia yangu tutafurahia siku hiyo kwa kufanya usafi mtaani kwetu Mikocheni na kuchangia utoaji damu ili kusaidia watu wenye uhitaji,” alieleza Mufti Zubeir na kuwataka Waislamu kutokujiingiza kwenye makundi ya ugaidi kwani Uislamu sio ugaidi na kuwasihi waachane na hizo tabia.
Post a Comment