Matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii yameendelea kulalamikiwa kuathiri mafanikio ya wanafunzi, licha ya kuwapo zuio wasiitumie wakati wa masomo.
Kilio cha hivi karibuni kuhusu mitandao hiyo ni cha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako aliyesema miongoni mwa changamoto zinazosababisha ongezeko la mmomonyoko wa maadili kwenye jamii ni pamoja na wanafunzi kutumia muda mwingi katika mitandao hiyo.
Profesa Ndalichako alisema wanafunzi wamekuwa wakitumia mitandao hiyo kwa kusoma, kuwasiliana na kusambaza picha zisizokuwa na maadili. Kwa hapa nchini mitandao inayopendwa na watu wengi ni Whatsap na Facebook.
Alisema kutokana na hali hiyo baadhi yao hafanyi vizuri katika masomo yao, hivyo kila mzazi, taasisi za kidini zinatakiwa kushiriki katika kusaidia kuondoa athari hizo.
Profesa Ndalichako alisema hayo jana wakati wa ufunguzi wa mdahalo wa wanafunzi wa sekondari za Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya ‘Kampeni ya Kitaifa ya Kujenga na Kukuza Maadili, Haki za Binadamu, Uwajibikaji, Utawala Bora na Mapambano dhidi ya Rushwa kabla ya kufikia kilele cha Siku ya Maadili nchini Desemba 10, mwaka huu.
“Lakini kuna changamoto kubwa kwa baadhi ya wazazi na walezi unakuta wanatetea watoto wao wanapofanya makosa na hawatoi ushirikiano, sasa kwa mazingira hayo tutakuwa tunajenga kizazi cha namna gani?” alihoji.
Alisema adhabu kwa wanafunzi zinatakiwa kutolewa kwa mujibu wa kanuni, taratibu na miongozo ya shule badala ya msukumo kutoka nje. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Binto Musa alisema mmomonyoko wa maadili unasababishwa na uwezo mdogo wa kuchambua athari mbaya na nzuri zinazotokana na utandawazi.
Mwalimu wa Sekondari ya Azania, Hamida Mgalu alisema mzazi na mwalimu wakishirikiana, wanafunzi watakuwa na maadili.
Post a Comment