0


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali haitawavumilia waajiri ambao hawatoi mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wao na amewaonya waache tabia hiyo mara moja.

Ametoa agizo hilo jana (Jumatano, Novemba 23, 2016) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Sita wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) katika ukumbi wa Mwalimu Julius K. Nyerere ulioko Chuo cha Mipango, nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Akijibu hoja ya waajiri kutokutoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi ambayo iliibuliwa kwenye risala yao, Waziri Mkuu alisema kifungu cha 14 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004  kinaelekeza aina mbalimbali za mikataba inayotakiwa kutumika kuajiri wafanyakazi. 

“Kisheria mwajiri anao wajibu wa kuhakikisha kila mtumishi wake ana mkataba wa kazi kwa maandishi,”alisisitiza.

Akijibu hoja kuhusu wafanyakazi kuwekwa ndani kiholela, kunyanyaswa, kushushwa vyeo na kusimamishwa kazi na wanasiasa, Waziri Mkuu alisema Serikali chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kuzingatia utawala wa sheria na kanuni za utawala bora ili kuhakikisha kuwa haki za wafanyakazi zinalindwa ipasavyo.

”Kimsingi watumishi wanasimamiwa na mamlaka za kinidhamu na sheria mbalimbali ambazo hazina budi kuangaliwa kwa pamoja kabla ya kuchukua hatua. Ninawaagiza viongozi wenzagu wa kisiasa na walioko katika wizara na taasisi zote za Serikali, mikoani, wilayani, kwenye idara za Serikali na Halmashauri wazingatie utawala wa sheria wakati wa kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusu wajibu na haki za wafanyakazi,” alisema huku akishangiliwa.

Akijibu hoja kuhusu suala la watumishi kutopandishwa vyeo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Bibi Angella Kairuki alisema kwa kipindi cha miaka mitano jumla ya watumishi 343,689 walipandishwa vyeo ikiwa ni kuanzia mwaka 2011 hadi 2016. Hata hivyo, alisema wanakabiliwa na changamoto ya watumishi wengine kutokidhi vigezo.

“Kuna baadhi ya watumishi hawakidhi vigezo vya maendeleo na masharti vya muundo wa masharti ya utumishi wa umma. Tumetoa maelekezo kuwa wale waliokosa vigezo na wamekaa muda mrefu bila kupandishwa vyeo, wapewe mafunzo na bajeti zitengwe ili waweze kutimiza vigezo vya muundo wa utumishi wa umma,” alisema.

Post a Comment

 
Top