Sakata la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuweka fedha katika akaunti maalumu kwenye benki za biashara limechukua sura mpya baada ya Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu kusema si kosa kisheria.
Profesa Ndulu, ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Bodi ya TRA iliyovunjwa na Rais John Magufuli Jumapili iliyopita, alisema mjini Arusa jana kuwa hakuna hasara kiuchumi kuweka fedha kwenye akaunti maalum isipokuwa hilo suala lilikuwa na hali nyingine.
Japokuwa Profesa Ndulu hakutaka kufafanua zaidi kwa maelezo lilichomekewa tu katika mkutano na waandishi wa habari wa kuelezea hali ya uchumi, alisema hali hiyo ndiyo suala lililozungumzwa na siyo kusema “fixed deposit account” ni mbaya.
“Kwani amesema fixed account zote ni mbaya, pamoja na za watu binafsi? Ndo hivyo sasa. Nilijua mtachomekea hilo kwa hiyo nilikuwa tayari,” alisema mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Profesa Ndulu alisema hayo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari walipotaka kujua athari za kiuchumi kwa taasisi za umma kuweka fedha kwenye akaunti maalumu tena benki binafsi.
Kauli hii ya Profesa Ndulu imekuja siku moja baada ya Rais Magufuli kueleza kilichochangia kuchukua uamuzi wa kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi, Bernard Mchomvu na pia kuivunja bodi yake iliyokuwa na wajumbe tisa. Kati ya wajumbe hao tisa, watano wanaingia kwa mujibu wa sheria na wanne ni wa kuteuliwa.
Wajumbe wanaoingia kwenye Bodi kwa mujibu wa sheria ni Gavana wa BoT, Profesa Beno Ndulu; Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata; Katibu Mkuu Wizara ya Fedha wa Jamhuri ya Muungano, Doto James; Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Zanzibar, Khamis Mussa Khamis; na Katibu Mkuu Mipango. Bodi hiyo ilivunjwa Jumapili iliyopita.
Rais Magufuli alisema juzi kuwa Bodi ya TRA iliyokuwa na watendaji hao wakuu wa idara na taasisi za Serikali ilifanya dhambi ya kuidhinisha uamuzi wa menejimenti kuweka mabilioni ya shilingi katika benki za binafsi.
“Juzi hapa tumekuta Sh26 bilioni zilizokuwa zimetolewa TRA kwa ajili ya matumizi ya TRA zikapelekwa kwenye mabenki matatu kama ‘fixed deposit account’ na bodi ikapitisha. Ndiyo maana nilipozipata hizo hela; hela nikazichukua na bodi kwaheri,” alisema Rais Magufuli alipokuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) yaliyofanyika mjini Kibaha mkoani Pwani ambako jumla ya watu 4038 walihitimu shahada mbalimbali
Ukwasi wa mabenki
Katika hatua nyingine Profesa Ndulu amesema ukwasi wa fedha katika mabenki umeshuka ikilinganishwa na kipindi cha nyuma hatua inayotatiza utoaji wa mikopo ya muda mrefu kwa ajili ya uwekezaji nchini.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mara baada ya kufungwa mkutano wa 18 wa taasisi za fedha uliofanyika kwa siku mbili jijini Arusha alisema hali hiyo inafanyiwa kazi na wadau wa taasisi hizo ili kuja na mbinu kufanya kuwa endelevu kwani uchumi unategemea uwekezaji unaotegemea mikopo ya muda mrefu.
Profesa Ndulu alisema BoT itahakikisha inaziwezesha benki kuendelea na jukumu lao la kutoa mikopo pia kuwa wabunifu wa kutafuta pesa kwa ajli ya amana badala ya kutegemea Serikali pekee.
“Benki zinaweza kukusanya amana kwa kiwango kikubwa lakini kama nilivyosema jana (juzi) kuwa katika kila Sh60 kati ya Sh100 zipo kwenye mikono ya watu badala ya kuwekwa akiba benki hivyo ni muhimu zikawekwa mbinu ya kuzipata kwa ajili ya kuwawezesha wawekezaji kuzitumia kwenye uzalishaji,” alisema.
Alisema katika kufanikisha mpango huo lazima kuvutia mitaji kutoka nje kwani hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kupiga hatua kwa kutegemea fedha za maendeleo na uwekezaji zitokane na mapato ya ndani pekee akitolea mfano wa China kuwa ni mfano uchumi wake kutegemea mitaji inayotoka nje ya nchi hiyo.
Katika hatua nyingine Profesa Ndulu alisema amekubaliana na wadau wa sekta ya fedha kuongeza nguvu katika kutoa mikopo na kuboresha mifumo ya taarifa kwa wale wanaotaka mikopo kwa ajili ya kilimo katika mnyororo mzima wa thamani kuanzia uzalishaji hadi kufika kwenye soko.
Profesa Ndulu alisema Tanzania imekaa vizuri kijiografia kufanya biashara na nchi zisizo na bahari zikiwemo Malawi, Uganda, DRC na Zambia katika kuwezesha sekta ya fedha kusaidia eneo la usafirishaji, bandari kufanya kazi na huduma kutolewa inavyotakiwa.
Mwenyekiti wa wenye mabenki ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei amesema waendeshaji wa mabenki wamenufaika na kuelewa mikakati na fursa za Serikali ambayo itawawezesha wao kutoa fedha kwa wafanyabishara.
Alisema wao kama CRDB wameweza kukusanya amana za Sh500 bilioni zinazokopeshwa kwa wafanyabiashara katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na kufungua matawi madogo madogo 100 nchi nzima.
Dk Kimei alisema serikali inapobanwa kifedha kutokana na kutegemea mashirika ya umma inawapa fursa sekta binafsi kupanua wigo wao kuwafikia wananchi wengi.
Post a Comment