Wanafunzi 1,132 wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), cha Mwanza hawatapewa matokeo yao ya kuhitimu shahada wala kushiriki katika mahafali baada ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kutolipa ada zao za mwaka huu wa masomo.
Kwa mujibu wa orodha ya wanafunzi iliyobandikwa katika ubao wa matangazo chuoni hapo, ni wanafunzi 933 tu watakaoshiriki katika mahafali yaliyopangwa kufanyika Desemba 16 na 17.
Tangazo hilo lililosainiwa na Makamu wa Mkuu wa Chuo (Taaluma), Dk Negussie Andre limewataka wanafunzi kuhakiki majina yao kwenye orodha na kuwasilisha malalamiko au hoja zao kabla au ifikapo Jumapili ijayo.
Kuhusu madai hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul Razaq Badru alisema hawezi kuyazungumzia kwa sababu kila chuo kina mamlaka yake.
Alisema Bodi hiyo ipo kwa miaka 10 na kwamba bila shaka kuna taasisi zinazoidai na zinalipwa kulingana na makubaliano na mipango iliyopo akisema kila wakati kuna malipo yanayoendelea katika vyuo mbalimbali.
Hata hivyo, alisema hana takwimu sahihi kama na chuo hicho kimeanza kulipwa.
“Tunafanya malipo kulingana na mipango iliyopo, kama kuna changamoto katika vyuo tunavyolipa au vinavyotudai huwa tunajadili kwa pamoja na kupata majibu, kwa hilo lililotokea Saut sisi kama Serikali hatuwezi kukemea wala kupongeza kwa sababu ni mamlaka ya chuo,” alisema Badru.
Akizungumza kwa simu jana jioni, Ofisa Mikopo wa Saut, Wilfred Medard alisema uamuzi huo umechukuliwa kutokana na malimbikizo ya ada ya wanafunzi wanaolipiwa na bodi hiyo.
“Siwezi kutaja ghafla ni kiasi gani tunachodai, lakini kwa hakika ni zaidi ya Sh500 milioni,” alisema Medard.
Alisema si rahisi kujua iwapo wanafunzi hao wote watashiriki mahafali kwa sababu bado kuna fursa ya bodi kulipa madeni hayo na kuwapa nafasi ya kushiriki mahafali na wenzao wanaojilipia au wanaolipiwa na kampuni, taasisi na mashirika mbalimbali.
Ingawa tangazo hilo limetoa hadi Jumapili ijayo kwa wahitimu ambao majina yao hayapo kwenye orodha kuhakiki na kuwasilisha taarifa zao, Medard alisema bado kuna fursa ya wahusika kukamilisha taratibu hadi Desemba 2 ambayo ni siku ya mwisho ya maandalizi ya mahafali.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi Saut (Sautso), Emmanuel Ayo alisema wanafunzi wanaunga mkono uamuzi wa chuo kuishinikiza Serikali kulipa madeni hayo ili kukiwezesha kujiendesha.
“Hiki ni chuo binafsi kinachojiendesha kupitia ada za wanafunzi. Kutolipa ada ni kukwamisha shughuli na masomo na sisi hatuko tayari kuona tunakosa masomo kwa sababu tu Serikali haitimizi wajibu wake wa kuwalipia wanafunzi inaowadhamini,” alisema Ayo.
Alisema iwapo muda uliotolewa na chuo kuhakiki utapita bila ya kulipwa kwa ada hizo, Sautso imepanga kuonana na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kuwasilisha kilio chao.
“Waziri asipotusaidia, tutakwenda hadi Ikulu kumwona Rais John Magufuli ambaye pengine wasaidizi wake hawampi taarifa sahihi kuhusu kinachoendelea Bodi ya Mikopo,” alisema Ayo.
Kiongozi huyo ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa shahada ya ualimu, alijitolea mfano kuwa ada yake ya muhula wa pili mwaka jana haijalipwa hadi sasa na bodi hiyo.
Post a Comment