Jeshi la Polisi mkoani Arusha jana asubuhi lilituliza vurugu za viongozi na wanachama wa Jumuiya ya Vijana ya CCM (UVCCM) mkoani hapa, waliokuwa wakigombea ofisi.
Vurugu hizo ziliibuka hadharani jana baada ya kuwapo taarifa za mgogoro wa chini kwa chini uliodumu kwa kwa miezi miwili, kati ya makundi mawili yanayokinzana kiuongozi.
Mgogoro huo ulielezwa kukolezwa na uhamisho wa Katibu wa UVCCM Mkoa, Ezekiel Mollel kwenda makao makuu, huku katibu mpya aliyepelekwa kuchukua nafasi hiyo akikwama kukabidhiwa kwa siku tatu sasa.
Katibu huyo mpya Saidi Goha, jana alitaka kuingia ofisini lakini alikumbana na kigingi cha kundi linalomuunga mkono Mollel lililofunga mlango kwa mnyororo. Kutokana na vurugu za jana, polisi wanamshikilia mwenyekiti wa miradi ya jumuiya hiyo, Phillemon Ammo pamoja na Mollel.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema: “Ni kweli tumemkamata lakini nina ugeni wa Serikali (wa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan), naomba nitoe taarifa baadaye,”alisema Mkumbo.
Lengai Ole Sabaya, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Arusha, alisema anapinga na kulaani kitendo cha baadhi ya wanachama wa umoja huo kufunga ofisi hizo kinyume na taratibu.
Lengai Ole Sabaya, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Arusha, alisema anapinga na kulaani kitendo cha baadhi ya wanachama wa umoja huo kufunga ofisi hizo kinyume na taratibu.
Mollel anadai uhamisho wake ni njama za kupoteza ushahidi wa baadhi ya tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya fedha kwenye jumuiya hiyo, hivyo hatokwenda popote.
Anasema yeye anatekeleza maagizo ya kamati ya utekelezaji ya kusimamia mali za chama, kwani katika kipindi cha miezi miwili ameokoa zaidi ya Sh30 milioni ambazo zilikuwa zinaingia mifukoni mwa watu wachache.
“Tuna maduka hapa, waliopangishwa wanalipa zaidi ya Sh300,000 lakini chama kinapata chini ya Sh50,000 kwa duka kama kodi ya mwezi sasa tumetaka wenye maduka kulipa moja kwa moja UVCCM na siyo kwa watu wa kati na hapa ndipo chanzo cha mgogoro,” alisema.
Kutokana na vurugu hizo zilizoibuka jana asubuhi, Sekretarieti ya UVCCM imeamua kumsimamisha kazi bwana Ezekiel Mollel.
Kaimu Katibu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka alitangaza uamuzi huo jana jioni muda mfupi baada ya Mollel kukabidhi ofisi kwa katibu mpya wa UVCCM mkoa, Saidi Goha ambaye amehamishiwa Arusha akitokea Lindi, akiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Baada ya makabidhiano hayo polisi walimrejesha kituo kikuu cha polisi anakoshikiliwa. Shaka alisema, Mollel aliandikiwa barua ya uhamisho kwenda makao makuu tangu Agosti 25, na alitakiwa kukabidhi ofisi ndani ya siku 14 lakini aligoma.
Alisema Mollel amekiuka kanuni za utumishi za UVCCM, hivyo Baraza Kuu na Kamati ya Utekelezaji Taifa watatoa uamuzi zaidi kwa mujibu wa kanuni kwa kuwa ukomo wa sekretarieti ni kumsimamisha.
Hata hivyo, Mollel akizungumza akiwa chini ya ulinzi, alisema makabidhiano hayo ni batili kwa kuwa hakuyasaini.
Hata hivyo, Mollel akizungumza akiwa chini ya ulinzi, alisema makabidhiano hayo ni batili kwa kuwa hakuyasaini.
Post a Comment