Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Lameck Nchemba amesema hakuna shamba lenye thamani ya maisha ya binadamu na kuwataka wakulima na wafugaji kutatua migogoro yao kwa kufuata sheria na kuacha kujichukulia sheria mkononi.
Mwigulu ameyasema hayo Bungeni jana wakati akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Mikumi kupitia (CHADEMA) Joseph Haule aliyetaka kujua hatua za serikali katika kudhibiti mauaji ya wakulima na wafugaji yanayotokea mara kwa mara katika jimbo lake na maeneo mengine nchini.
Katika swali lake Mbunge Haule ametaja baadhi ya mifano ya mauaji katika jimbo lake hususani eneo la Tindiga ambapo mauaji yamekuwa yakifanyika mara kwa mara huku serikali ikitoa matamko ambayo hayajazaa matunda.
Waziri Mwigulu Nchemba amesema katika kijiji ambacho mauaji yatafanyika jeshi la polisi litakamata vijana wote wenye nguvu na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ili wahusika waweze kubainika.
“Naliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata vijana wote wenye nguvu katika kijiji ambacho mauaji yatafanyika ili wahusika wapatikane na kama magereza zikijaa vibaka walioiba vitu vidogovidogo waachiwe ili hao ambao wamesababisha mauaji wawekwe humo hatuwezi kufananisha maisha ya binadamu na mifugo au shamba” Alisema Waziri Mwingulu.
Awali katika swali hilo Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Dkt. William Ole Nasha aliwataka wafugaji na wakulima kuepuka kutumia hasira ambazo zinapelekea kugharimu maisha ya watu kwani serikali haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria.
Post a Comment