WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na wawekezaji wa kampuni tisa za nchini Korea Kusini na kumuahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuwekeza katika sekta ya kilimo, viwanda, maji, miundombinu, elimu, afya na michezo.
Wawekezaji hao wanatoka kampuni ya Sima textile, ESM, Jusung Solar Engineering, Seongnam City FC, Yeong Yang City Korea,Ulsan Vocational Training, Egis Smart City, MBN
Akizungumza na wawekezaji hao jana jioni (Jumanne, Septemba 27, 2016) kwa niaba ya Mhe. Rais Dk. John Magufuli, Waziri Mkuu alisema kwamba Tanzania ni sehemu salama kwa uwekezaji ikiwa na fursa za uwekezaji kwenye sekta nyingi kama miundombinu, kilimo na viwanda. Licha ya mazingira mazuri ya uwekezaji pia aliwahahakishia ulinzi kwenye uwekezaji wao.
Waziri Mkuu alisema Korea ya Kusini inashirikiana vizuri na Tanzania hivyo wanatarajia mengi kutoka nchini huko kupitia wawekezaji hao.
Wawekezaji hao tayari wamefanya mazungumzo na viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijinii Mwanza na kusaini Hati ya Makubaliano (MoU) kwa ajili ya miradi minne ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu ya maji, kiwanda cha nguo, zana kubwa za kilimo na mafunzo ya ufundi.
Kwa upande wake Mkuu wa Msafara huo, Bw. Son Young Soo alisema amefurahishwa na ziara waliyofanya nchini na wapo tayari kuwekeza nchini.
Naye, Bw. Jihyun Kim wa kampuni ya Yeong Yang City Korea ambayo inashughulikia masuala ya kilimo cha mbogamboga alisema watawekeza kwenye kilimo hususan cha zao la pilipili na watajenga kiwanda kwa ajili ya usindikaji.
Naye Mkurugenzi wa Klabu ya Soka ya Seongnam Bw. Suk Hoon Lee alisema klabu yake ipo tayari kuwekeza katika shule ya michezo kwa vijana ili kuongeza kasi ya maendeleo ya soka.
Post a Comment