0
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa rai kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, kuvunja mkataba uliopo katika mradi wa Machinga Complex ili kuokoa fedha za wananchi zinazopotea kupitia mkataba huo.

Makonda alitoa rai hiyo jana jijini hapa alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu tathmini ya mkataba uliopo katika mradi huo baada ya Simbachawene kumkabidhiwa asimamia jengo.

Alisema mkataba uliopo kati ya Jiji na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) hauridhishi hivyo amemuomba waziri huyo kuuvunja mkataba huo na kuchukua eneo hilo kwa makubaliano ya kwamba Halmashauri ya Jiji walipwe kodi ya ardhi, jambo ambalo linaweza kufanyika kwa urahisi kupitia NSSF na Jiji kumiliki hisa kwa pamoja.

Makonda alisema shirika hilo liliingia mkataba wa mkopo wa Sh bilioni 10 na Jiji kwa kujenga jengo la Machinga Complex lenye ghorofa tano na ghorofa sita ili liweze kumudu idadi ya machinga 10,000 lakini hali halisi baada ya kulitembelea jengo lina ghorofa nne zinazobeba machinga 4,000 tu.

“Tulivyopitia mkataba tuligundua kuwa una mapungufu mengi na huenda ulisainiwa na watu ambao walipofushwa na rushwa na kukubali kupoteza haki za wanyonge,” alisema Makonda.

Alisema baada ya kupitia mkataba huo pia amebaini kuwa fedha za mikopo ziliongezeka kutoka Sh bilioni 12.14 za kwenye mkataba na kufikia Sh bilioni 12.7 ikiwa ni nyongeza ya Sh milioni 560, ambayo ilifanyika bila makubaliano yoyote kati ya mkopeshaji na mkopaji hali ambayo haimtendei haki mkopaji.

“Mei 25, 2010 walikabidhiwa jengo likiwa linadaiwa riba ya Sh bilioni saba hivyo siku ya kwanza ilikuwa tayari inadaiwa jumla ya Sh bilioni 19.7 na hadi kufikia Machi mwaka huu deni lilikuwa Sh bilioni 38 lakini mpaka sasa wamelipa Sh milioni 50,” alisema Makonda.

Alisema shirika hilo lilianza kudai riba kinyume na mkataba ambao unaeleza kuwa riba italipwa baada ya miaka miwili.

Alisema katika hali ya kushangaza shirika hilo halikutoa fedha za mradi kwa Jiji na badala yake kubadilishwa utaratibu wa kifungu kidogo cha mkataba namba 4.1 kwa kusema anayekukopesha ana jukumu la kuchukua fedha na kukutana na mshauri wa mradi pamoja na mjenzi na shirika kumlipa.

Post a Comment

 
Top