0
Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa Kijiji cha Sanaa maarufu kama Dagaadagaa ambao vibanda vyao vya kuuzia nyama ya nguruwe na vinywaji vilivunjwa juzi, kwa amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wamesema ubomoaji huo umewasababishia hasara.

Wakizungumza jana, walisema walikuwa wameandaa nyama hiyo kwa ajili ya kuchoma na kukaanga, lakini walishindwa kufanya hivyo baada ya kushtukizwa na ubomoaji wa vibanda.

?Ni hasara kubwa tumepata, hata haiwezi kuelezeka. Nilikuwa na ?oda? ya nyama kilo 90 ambayo thamani yake ni Sh900,000,? alisema mmiliki wa moja ya vibanda vilivyovunjwa, Alexander Rangi.

Rangi alisema baada ya kuvunjiwa kibanda chake nyama hiyo ilibaki ndani ya friji na hajui ataipeleka wapi kwa kuwa hana eneo jingine la kuuzia.

Masawe Robert alisema alikuwa ameagiza kreti 100 za bia, soda na vinywaji vingine, lakini vyote viliharibikia ndani ya banda wakati wa bomoabomoa.

?Sikuwa na taarifa, nikashangaa greda linafika kwangu. Kwa kweli ni hasara siwezi kuielezea kabisa,? alisema.

Ubomoaji wa eneo hilo ulikuja baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa amri ya kuvunjwa kufuatia ushindi wa M/S Cool Makers Limited dhidi ya Jumuiya ya Wazazi na John Ondoro. Mgogoro huo ulianza tangu mwaka 1993.

Walimiki wengine wa vibanda walisema ubomoaji huo umesababisha kupotea kwa taswira ya kibiashara kwa kuwa eneo hilo lilikuwa likiwapatia wateja wengi.

?Hapa huwa wanajaa watu kila siku haijalishi ni mchana, usiku au asubuhi. Kwa hiyo tangu jana hatujauza chochote,? alisema Festo Fantaleo.

Katika hatua nyingine, baadhi ya kaya zilizokuwa jirani ambazo zilivunjiwa nyumba zilidai kutojua chochote kuhusu uvunjwaji huo, kwa kuwa hazikujua kama eneo hilo lilikuwa na kesi mahakamani.

?Sikujua chochote nilijua tuko eneo salama na mimi nilinunua kwa mtu, tena kwa mkopo wa vicoba kwa Sh15 milioni na nimejenga nyumba kwa mkopo wa vicoba,? alisema Dionisia Mchamba.

Mchamba alisema ana zaidi ya miaka 15 anaishi eneo hilo na hakuwahi kuelezwa chochote wala kupewa taarifa za ubomoaji.

Wakati mwandishi wa gazeti hili akiwa eneo hilo alishuhudia ujenzi wa uzio ukiendelea chini ya ulinzi mkali wa Kampuni ya Uwazi Security, huku wenye vibanda vilivyovunjwa wakitakiwa kuondoa vitu haraka.

Mmoja wa wasimamizi wa eneo hilo kutoka Kampuni ya Udalali ya Mem Auctioneers and General Brokers, Jophrey Kiua alisema wameimarisha usalama na kuruhusu watu kuondoa vitu vyao ili waweke uzio. 

Post a Comment

 
Top