Ni nani aliyemuingiza shimoni mwanamke huyo na kwa madhumuni gani? Kwani kwa jinsi shimo lilivyo, lazima aliingizwa au aliingia kwa kutumia ngazi.
Alikuwa akiishi kwa kula chakula gani kwani wakati anatolewa, muda mwingi alikuwa akilalamikia njaa.
Swali la tatu ambalo majirani walikuwa nalo, mwanamke huyo aliishi ndani ya shimo hilo kwa siku ngapi? Kwani nywele na kucha zake ziliashiria si zaidi ya mwezi mmoja. Swali kuu, aliingia/ aliingizwa lini na muda gani kati ya mchana na usiku?
Je, aliingizwa kwenye shimo hilo akiwa na nguo zake halafu aliyemwingiza/ waliyomwingiza walizipeleka wapi?
Swali la tano ambalo majirani hao walikuwa wakilijadili sana ni, je! Mwanamke huyo ni mgonjwa wa akili au ni msukule? Kama si chochote kati ya hayo mawili, kwa nini alikuwa hapigi kelele?
Sita, majirani hao waliulizana kama siku za karibuni wamewahi kusikia kwenye vyombo vya habari kuna mwanamke mwenye umri huo anatafutwa? Wote walisema hawajasikia.
Wengi walisema huenda mwanamke huyo aliingizwa kwenye shimo hilo na ‘maadui’ wa biashara wa Mtei. Lakini kama ni kweli, walikuwa na lengo gani na walimpata wapi mwanamke huyo na akiwa katika hali gani?
Katika mahojiano na majirani wakati bado akiwa ndani ya shimo amekaa, mwanamke huyo aliweza kujibu maswali karibu yote, lakini swali la anaitwa nani na ameolewa au la, yalimshinda kujibu. Ni kwa nini?
Polisi Mbezi wanasema wamekuwa wakimpigia simu Mtei, lakini hapokei. Ni kwa nini?
Naye mfanyakazi anayeitunza nyumba hiyo, Richard Pascal alipozungumza na Uwazi kuhusu tukio hilo alikuwa na haya:
“Ninachokumbuka mimi, Jumanne, wiki iliyopita, saa 3:00 asubuhi, bosi wangu Mtei alikuja. Ni kawaida yake kuja na kukagua mji wake.
Nikiwa naendelea na shughuli zangu, aliniita hapa nje. Nilipofika aliniambia nichungulie ndani ya shimo. Nilifanya hivyo, nikashtuka sana kumwona mwanamke akiwa mtupu huku akinikodolea macho.
“Niliogopa kwa sababu sikutarajia kama kuna mtu anaishi shimoni bila mimi kujua wakati ndiyo nalinda hapa siku zote.”
AWAITA MAJIRANI
“Niliamua kuwaita majirani. Baada ya muda mfupi watu wakawa wamejazana hapa kila mmoja akishangaa na bosi wangu akatoa taarifa Kituo Kidogo cha Polisi Kibamba ambapo askari walifika.
“Lakini na wao walipatwa na mshangao huku wakijiuliza ni vipi mwanamke huyo aliingia shimoni bila kuumia wala kuvunjika?”
POLISI WAMUHOJI
“Mwanamke huyo alipohojiwa na polisi alisema ameishi humo miaka mingi na mara nyingi alipokuwa akihojiwa alikuwa akililia chakula. Polisi waliniomba ngazi, wakaitumbukiza shimoni kisha yeye mwenyewe akapanda haraka mpaka nje.”
APELEKWA TUMBI
“Polisi walimchukua na kumpeleka Hospitali ya Tumbi (Kibaha mkoani Pwani) ambako nadhani anapatiwa matibabu.”
MLINZI APATA WASIWASI
“Mpaka sasa hivi mimi napatwa na wasiwasi. Nitamuomba bosi wangu aniongezee mtu mwingine ili tuwe wawili, kwani mimi hapa ni mgeni. Nimekuja hapa, Desemba 9, mwaka jana.”
SIKILIZA MAHOJIANO
Uwazi lilifanikiwa kunasa mahojiani kati ya mwanamke huyo akiwa ndani ya shimo amekaa na polisi huku wananchi wakiwa nje wakitaka kumuokoa.
Polisi: “We, unaitwa nani?”
Mwanamke: (kimya).
Polisi: “Unakaa wapi?”
Mwanamke: “Mbezi Makabe.”
Polisi: “Umeolewa?”
Mwanamke: (kimya).
Polisi: “Umekuja lini hapo?”
Mwanamke: “Hapa kwangu.”
Polisi: Umekuja lini?”
Mwanamke: “Mi njaa inaniuma bwana.”
UWAZI NYUMBANI ANAKOISH
I MTEIUwazi lilifika nyumbani kwa Mtei, Kibamba ya Luguruni jijini Dar, hatua chache tu kutoka kwenye Kituo cha Mabasi Kibamba lakini hakupatikana, Uwazi liliacha namba ya simu lakini hakupiga na ilipopigwa, imekuwa ikiita bila kupokelewa.
UWAZI KITUO CHA POLISI
Siku hiyohiyo, Uwazi lilifika Kituo cha Polisi Mbezi ambapo askari mmoja ambaye hakupenda kutaja jina lake kwa vile si msemaji wa jeshi hilo, alisema mpaka sasa wanamtafuta Mtei ili kumsikia kwa kina kuhusu tukio hilo kwa vile yeye ndiye aliyepiga simu polisi kutoa taarifa.
“Huyo Mtei, tunamtaka hapa. Yeye ndiye aliyetoa taarifa ya mwanamke kukutwa kwenye shimo nyumbani kwake. Lakini tulipofika hatukumkuta. Na kila tukipiga simu yake, inaita tu bila kupokelewa,” alisema afande huyo.
UWAZI HOSPITALINI TUMBI
Baada ya hapo, Uwazi lilifunga safari hadi Hospitali ya Rufaa ya Tumbi, Kibaha, Pwani ambapo halikufanikiwa kumpata msemaji, lakini muuguzi mmoja wa hospitali hiyo alikiri kupokelewa kwa mwanamke huyo.
UWAZI LAMBANA MTEI
Juzi, Uwazi lilimpigia simu Mtei na mambo yakawa hivi;
Uwazi: “Wewe ni Mtei?”
Mtei: “Eee, unasemaje?”
Uwazi: “Tunaomba ufafanuzi kuhusu yule mwanamke aliyekutwa kwenye shimo nyumbani kwako…”
Mtei: “Ooh! Siyo mimi, yule ni Mchaga mimi ni Muhaya, nipo Kagera.”
Uwazi likamrudia aliyetoa namba…
“Kwani si ulikuwa unaongea naye sasa hivi na akakwambia yeye si Mtei! Nimesikia maongezi yenu, lakini alisogea mbali. Kwa hiyo sijui zaidi.”
KAMANDA WA POLISI KINONDONI
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Christopher Fuime alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alikiri kulitambua na kwamba, bado wanalifanyia uchunguzi.
Yeyote anayemjua mwanamke huyo (pichani ukurasa wa mbele) apige simu namba 0715454656 au 0784 339616, chumba cha habari.
Post a Comment