BAADA ya timu ya vijana ya Stand United kupokea kipigo cha mabao 4-0 juzi Jumapili, imebainika kwamba Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Mfaransa Patrick Liewig amegoma kupeleka kikosi cha wakubwa kushiriki michuano maalumu kwa timu za Kanda ya Ziwa zinazocheza Ligi Kuu Bara.
Mfaransa huyo ameuambia uongozi kwamba bado kikosi chake hakijajengeka kwa mashindano hivyo kugoma kuipeleka timu kupata aibu na badala yake jukumu hilo akaliacha kwa timu ya vijana chini ya miaka 20 ya Stand.
Kikosi hicho cha U-20 cha Stand kilikutana na dhahama ya kufumuliwa na Mwadui FC iliyo chini ya kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ katika mechi iliyochezwa katika Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Ofisa Habari wa Stand United, Deo Makomba, ameliambia Mwanaspoti kuwa Liewig ametoa programu yake kuwa ataanza kucheza mechi za kirafiki baada ya siku kumi tangu timu hiyo ilipoingia kambini juzi Jumapili katika mgodi wa Buzwagi uliopo Kahama mkoani humo.
“Tunaheshimu mashindano hayo ila kocha amesema kuwa bado anatengeneza kikosi hivyo asingeweza kuipeleka timu ya wakubwa kwenye mashindano hayo,” alisema Makomba.
Post a Comment