0
Ndugu zangu,
Juzi hapa kwenye siku yake ya kuzaliwa, Rais wa Awamu ya Tano, Dr John Pombe Magufuli yumkini aliacha kula keki yake ya kusheherekea siku yake hiyo na kuamua kuwa kazini.
Zikatujia taarifa kubwa mbili; utenguzi wa uteuzi wa DCI na ziara ya kushtukiza wizara ya Maliasili na Utalii.

Nataka niwe mkweli kwa nafsi yangu, kuwa hata kama tungekuwa, kama nchi, na utaratibu wa kuwa na Rais wa kipindi cha mwaka mmoja, basi, huyu tuliye naye sasa, John Pombe Magufuli, angekuwa amemaliza muda wake wa mwaka mmoja akiwa ameacha alama nyuma yake, alama za kudumu muda mrefu.

Ukweli nchi yetu imeanza kubadilika na fikra za watu wake pia zimeanza kubadilika. Maana, ilifika mahali, kuna walioacha kazi kwenye NGO- Mashirika yasiyo ya Kiserikali na kwenda kufanya kazi Serikalini ikiwamo kwenye Halmashauri zetu wakitamka wazi kuwa kwenye NGO kazi nyingi, wanarudi Serikalini na kwenye Halmashauri kupumzika na kula posho za safari na nyinginezo.
Nchi haiwezi kusonga mbele ikiwa na watu wenye mitazamo kama hiyo. Ni lazima kuwe na nidhamu ya utendaji kazi na kuheshimu sheria, kanuni na taratibu. Na wenye kukiuka hayo, ni lazima wajue kuna adhabu yenye kuendana na matendo yao maovu. Ndiyo siri kubwa ya nchi za wenzetu zilizoendelea.


Nilipata kuandika hapa, kuwa inavyoonekana; Magufuli Ana Uwezo Wa Kumwona Bata Na Sungura Kwa Wakati Mmoja..! ( Novemba 30, 2015)
Hii ni dhana kongwe ya kimtazamo iliyojengeka kifalsafa. Ni uwezo wa mwanadamu katika taswira moja kuwaona viumbe wawili wenye kufanana. Hivyo, inahusu uwezo kuliona jambo hilo hilo katika sura tofauti.

Ndio, kuna kuona kikiwa na kuona kama. Kuliangalia jambo kwa mtazamo tofauti.
Mwanafalsafa Thomas Kuhn yeye anazungumzia dhana ya ' Paradigm Shift'. Ni ile hali ya uwepo wa mapinduzi ya kifikra na ya kisayansi yenye kupelekea mabadiliko ya kimsingi katika jambo lile lile tulilokuwa na mazoea nalo.

Captain Thomas Sankara, kiongozi mwanapinduzi aliyeuawa wa Burkina Faso, katika wakati wake, alizungumzia umuhimu wa kuwa na ujasiri wa kuyapa mgongo mazoea ya kale.
Sankara aliacha hiba njema ya kuenziwa ndani ya nchi yake, Afrika na duniani. Mwanamapinduzi huyu alikuja kuawa kwa kupigwa risasi na wapinga mapinduzi na maendeleo ya Burkina Faso.
Sankara alipata kukaririwa akisema: “Ningependa kuacha nyuma yangu, imani ya kuwa, kama tunaimarisha kiwango fulani cha uangalifu na oganaizesheni, basi, tunastahili ushindi.

Kamwe huwezi kuleta mabadiliko ya kimsingi bila ya kuwa na kiwango fulani cha uwendawazimu. Hali hii inatokana na kutoshinikizwa na taratibu zilizozoeleka, kuwa na ujasiri wa kuzipa mgongo kanuni za kizamani, ujasiri wa kuanzisha mustakabali. Ni wendawazimu wa jana waliotuwezesha kuyafanya tuyafanyao leo. Ninataka kuwa mmoja wa wendawazimu hao.” (Hayati, Kapteni Thomas Sankara)

Yumkini tunachokishuhudia kwenye nchi yetu ni Magufuli's paradigm shift'. Hali ya kuwa na mabadiliko ya msingi.
Na hii ya Magufuli paradigm shift inaweza kuibadili nchi kwa haraka, maana kila mmoja atalazimika kubadilika.
Maggid,
Iringa

Post a Comment

 
Top