0
Mahakama ya wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, imemkuta na hatia ya Judith ‘Lady Jaydee’ Wambura katika kesi iliyofunguliwa dhidi yake na Clouds Media Group miaka takriban mitatu iliyopita.
14449334_1820386108190547_3689471538278432768_n
Hukumu hiyo imetolewa Jumatano hii (November 2) na Hakimu Boni Lyamike. Katika kesi hiyo, Lady Jaydee alifunguliwa mashtaka na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Joseph Kusaga pamoja na Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji, Ruge Mutahaba ya kuwachafua/kuwakashfu kupitia blog yake.
Hakimu huyo amemwamuru Lady Jaydee kuwaomba wawili hao radhi kupitia vyombo vya habari kwa kuchafua taswira zao na pia kuwalipa fidia kutokana na madhara waliyoyapata. Jide atatakiwa kulipa gharama za wanasheria ilizotumiwa na Clouds Media kwenye kesi hiyo.
Jaydee aliyekuwa shahidi pekee kwenye kesi hiyo alikiri kuandika maneno ya kuwachafua Kusaga na Ruge kupitia blog yake.
Moja kati ya maneno yaliyomtia hatiani Jaydee ni wosia aliouandika May 2013 kupitia blog yake.
Wosia huo ulisomeka:
Watu wanashtuka mtu akiongelea kifo, Utafikiri hawafahamu fika kuwa kila nafsi itakionja, Kwenye maisha yangu nimepitia mambo mengi, magumu na mepesi. Na bado naendelea ku experience mambo magumu zaidi kadri ninavyozidi kuwa mkubwa.
Siku za karibuni nimekuwa nikipigwa vita sana na watu wenye uwezo mkubwa kifedha , ki umri na hata wenye ukubwa wa connection katika hii industry ya muziki. Wanaomiliki chombo cha habari. Nasimama na kusema kuwa sitokata tamaa, kwani lengo lao kubwa ni kuona na kuhakikisha nimeanguka kabisa na sipo katika ramani ya muziki.
Watu hao ambao vita yao ilikuwa baridi miaka kumi iliopita, sasa inazidi kuwa moto baada ya kutambua kuwa mimi ni mtu mwenye maamuzi yangu na misimamo yangu bila kuburuzwa. Wanapita kila mahali kuhakikisha kila mrija unaoniingizia chochote unakatika, na hiyo ni kutaka kuuthibitishia umma wa Tanzania kuwa hakuna msanii anaeweza ku survive bila wao.
Mimi ni msanii tofauti na hao mnaofikiria. Nadhani mnafahamu tangu niachane na Tuzo zenu mnazo influence nani apate nani asipate, na tangu niachane na Fiesta nilipolipwa laki 8 mara ya mwisho na kuamua kuunda Band ili nijiajiri na kupata shows zangu mwenyewe, ikafanikiwa sana jambo ambalo limewauma na kuamua kufanya kitu cha kuiangusha Band yangu.
Nita survive kwa njia zozote MUNGU alizonipangia. Wakati bado wote tunapumua na kwakuwa watu hao hawanipendi kabisa, Naamini fika hawataweza kunipenda hata siku nitakapokuwa nimekufa. Na huu ndio wosia wangu kwa watu hao. Natambua wanaweza kutumia redio yao kutangaza sana kifo changu na kusema marehemu alikuwa mtu mzuri na pengine kupiga nyimbo zangu kuanzia asubuhi mpaka jioni.
Ila naomba nitamke hivi, siku nikifa CLOUDS FM isipige nyimbo zangu, wala isiongelee lolote kuhusiana na kifo changu. Ruge Mutahaba na Joseph Kusaga wasihudhurie msiba wangu, na mkiwaona muwapige. Enyi mtakaokuwa hai baada yangu. Kama wamenifitini, na hawajanipenda nikiwa hai. Hakuna haja ya kujifanya kunipenda nikiwa marehemu. Sina haja wanipende pia kwakuwa mimi sio ndugu yao, Ila ubaya wanaoundeleza mioyoni mwao wanaujua na nina hakika nafsi zao zinawasuta pia.
Niliamua kujiepusha nao miaka mingi na kufanya biashara zangu, nimekaa kimya watu wanafikiri nabebwa lakini sijabebwa chochote sikutaka ugomvi haya mambo yalianza baada ya Album yangu ya pili ya Binti mwaka 2003 nilipojitoa Smooth Vibes chini ya Ruge.
Nilivumilia fitna nikiamini ipo siku yatakwisha lakini naona moto ndio unazidi kuwaka. Na hii ni kwasababu wanaogopa msanii akiwa mkubwa watashindwa kumuamrisha, Hamuwezi kumiliki dunia..
Kama mnasema mlinibeba mbona hamkuwabeba dada zenu wa tumbo moja waimbe ili hela irudi nyumbani??. kama kweli wewe Kusaga unajua kubeba basi beba jiwe liimbe liwe star..
Kwa roho zenu mbaya mnaweza kumbeba mpita njia nyie??.
Talent haibebwi, hujibeba kama mnabisha si mna watoto wabebeni basi wawe kama kina Diamond ndio nitaamini kweli nyie mnaweza kubeba watu. Mnawatishia wasanii kuwa yoyote atakaefanya nyimbo na mimi hazitapigwa, vikao vinne mmeshakaa kunijadili. Mnadhani je! nitapungukiwa nini endapo wasanii wengine wakiacha kufanya kazi na mimi?? nyimbo hazitakuwa nzuri.
Basi sawa ngoja tuone MUNGU ni nani, Binadamu nani?? Kwahiyo mtaamrisha watu pia wasikae na mimi?? Ilikuwa niseme majina matatu huyo mmoja nimemsamehe baada ya kugundua sio hiyari yake ila yuko under influence ya hawa jamaa wawili. Kila siku mnamsingizia Ruge peke yake Kusaga ni mfitini kuliko hata huyo Ruge, watu hamjui tu. Mtu hela zote hizo bado shillingi mbili ya Jide inakuuma?? Roho gani hiyo?? Naishia hapo na sitabatilisha kauli yangu
Meneja wake, Seven Mosha, ameiambia Bongo5 kuwa Lady Jaydee atatoa maelezo yake kuhusu hukumu hiyo muda si mrefu.
January 8, 2014, Ruge alizungumza kupitia kipindi cha Power Breakfast kuhusu tuhuma mbalimbali alizowahi kutupitiwa na Jide ikiwemo hila za kuipoteza bendi yake ya Machozi.
Alisema anasikitishwa na jinsi Jaydee anavyoendesha harakati zake na kudai kuwa anapigana kwenye vita isiyo sahihi.
“Jaydee akaze buti, anapigana na wrong war, vita yake ameidirect tofauti na mizinga yake, bunduki zake amezielekeza kusiko. Skylight Band inamsumbua, akubaliane na ukweli kwamba Skylight ndio iliyoisababishia Nyumbani Lounge kushuka ilivyoshuka, sio Lady Jaydee kama msanii. Vita yake na bunduki zake azielekezee Skylight Band. Hajazungumza hata mara moja kwamba ndio kitu kinachosumbua. Mimi naamini kabisa akifanya hiyo kazi, Jaydee bado ni msanii mzuri, ana nguvu, afanye kazi kubwa ya kuweza kurudisha mapambano yake kisanii, kufanya kazi na aangalie tatizo lililotokea Nyumbani Lounge labda anaweza akatatua matatizo lakini sio kushambulia watu kwenye mitandao,” alisema Ruge.
Pia alisema yupo tayari kukaa meza moja na Lady Jaydee kuzungumza na kumaliza tofauti zao.
“Mimi niko tayari, kesho, kesho kutwa, kama yupo tayari na ana watu wengine wengi tu ambao wanahisi kuna matatizo binafsi ya kuongea na Clouds, twende sehemu nyingine neutral tu, tukodishe, tukae pale tusikie matatizo. Haisaidii muziki wetu kuonekana Bongo Flava ni watu ambao kutwa ni kulalamika, kutwa ni maneno na matusi tu pale panapokuwa na matatizo.”

Post a Comment

 
Top