Jiji la Mbeya ni la pili kwa wingi wa madhehebu barani Afrika likiongozwa na Lagos lililopo Nigeria.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika, jiji hilo lina makanisa 450 na Mtaa wa Sae pekee una madhehebu tisa huku Mtaa wa Simike ukitajwa kuongoza kwa vituo vya maombezi.
Meya wa Jiji la Mbeya, Mchungaji David Mwashilindi ambaye ni kiongozi wa Kanisa la International Evangerism Assemblies of God, amesema migogoro ndani ya madhehebu, uroho wa madaraka na utapeli ni miongoni mwa sababu ya watu kuamua kuanzisha madhehebu kila kukicha.
Meya huyo ambaye pia ni msimamizi wa kanisa hilo katika mikoa ya Ruvuma, Iringa, Njombe na Rukwa, amesema hakuna ubaya wa kuwa na madhebu mengi kama yanaanzishwa kwa kufuata utaratibu, sheria na misingi ya Mungu.
Amesema madhehebu mengi ya kilokole jijini humo yaliibuka baada waamini kuamua kujitenga madhehebu yao ya awali kutokana na migogoro.
“Kuna madhehebu yanamiliki vyuo vya wachungaji wanaosomea kwa mujibu wa maadili ya Mungu, kama Lutherani, Wakatoliki, Moravian, Wasabato na la kwangu, lakini tatizo wapo wachungaji wa kujipachika ambao mara nyingi wanatiliwa shaka kwa vitendo vyao,” amesema meya huyo.
Post a Comment