WAZIRI MKUUkuu Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wiki moja kwa Afisa Elimu Mkoa wa Pwani, Yussuph Kipengele kupeleka walimu wa kufundisha masomo ya kidato cha tano na sita katika shule za sekondari za Mkongo na Utete wilayani Rufiji.
Ametoa agizo hilo Jumatatu, Septemba 26, 2016 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Jumba la Maendeleo wilayani Rufiji. baada ya Mbunge wa Rufiji, Muhammed Mchengelwa kumwambia kuwa wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa walimu wa kidato cha tano na sita licha ya kuwa na shule.
"Hatuwezi kuwa na shule ambazo hazina walimu, nasikia hapa anayefundisha ni Mkuu wa shule na mwalimu mmoja tu, wakati kule Kibaha kuna walimu walmerundikana ,sasa fanya realocation tarehe 4,Oktoba uniletee taarifa walimu wamefika Rufiji.",alisema Waziri Mkuu.
Akizungumzia suala la upungufu wa watumishi wa umma kwenye sekta mbalimbali, Waziri Mkuu alisema baada ya kazi ya uhakiki watumishi hewa itakapokamilika, serikali itaangalia kwenye maeneo yenye upungufu na hivyo kutangaza ajira.
"Hivi sasa serikali inakamilisha masuala ya uhakiki wa watumishi, tukimakamilisha na kujua idadi ya watumishi na maeneo yenye upungufu tutaanza tena kuajiri, tulisitisha kupisha kwanza kazi hii,alisema Waziri Majaliwa.
Kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji Waziri, Mkuu alisema watendaji wa halmashauri na vijiji wanapaswa kutenga maeneo ya wafugaji na wakulima na kutaka mifugo isiongezwe kwenye maeneo ambayo hayajaruhusiwa.
Alisema wenyeviti wa vijiji wanapaswa kusimamia utekelezaji wake katika mpango wa matumizi bora ya ardhi na kwamba atakayeruhusu idadi kubwa ya mifugo kuingia kijijini zaidi ya ile iliyokubalika atawajibishwa ikiwemo kufukuzwa kazi na hatua nyingine za kisheria.
"Hatuwezi kuendelea kuwa na watumishi wasio na nidhamu, wale wote watakaoingia mifugo zaidi ya uwezo wa kijiji wafukuzwe kazi na kuchukuliwa hatua, lakini pia wafugaji ni marufuko kuingiza mifugo kwenye mazao ya wakulima"alisema Waziri Mkuu.
Kuhusu ujenzi wa barabara ya lami kwenda makao makuu ya wilaya ya Rufiji, Utete, Waziri Mkuu aliahidi kuchukua ombi hilo na kusema bajeti ijayo litatengewa fedha kuwa ajili ya kufanya maandalizi ya upembuzi kuona gharama yake kabla ya kutangaza zabuni ya ujenzi.
Kuhusu utengenezaji wa madawati, Waziri Mkuu alisema ifikapo Oktoba 30, mwaka huu kila wilaya nchini inapaswa iwe imekamilisha utengenezaji wa madawati hayo kwenye shule nchini.
Aidha, alisema ipo miradi mingi inayoendeshwa kwa maslahi binafsi ukiwemo mradi wa Bonde la Rufiji(RUBADA), ambao wamebaini kuna ubabaishaji mkubwa, hivyo wamepeleka timu ya wataalamu kuhakiki ili wale wabadhirifu wachukuliwe hatua.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, SEPTEMBA 26, 2016
Post a Comment