0
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnaye
Dodoma/Dar. CCM imesema haitarudia makosa ya mwaka 2010 ya kutengua uamuzi wa wanachama, lakini itahitaji kuwa na moyo mgumu baada ya makada wengi kukata rufaa kupinga matokeo ya kura za maoni.
CCM inamalizia hatua ya mwisho ya mchakato wake wa ndani wa kupata wagombea ubunge na udiwani kwa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu vitakavyopitia majina ya makada wote walioshinda kwenye kura za maoni, ambazo zilitawaliwa na tuhuma za rushwa na ukiukwaji wa taratibu.
Vikao hivyo huwa vinaweza kutengua ushindi wa kada kwenye kura za maoni kwa kuangalia rufani zinazopinga mchakato, tuhuma za rushwa na ukiukwaji wa taratibu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema wamepokea malalamiko mengi kuhusu ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi katika upigaji wa kura za maoni.
“Kumekuwa na utamaduni wa kulalamika barabarani wakati mwingine kushawishi wanachama kulalamika kwenye vyombo vya habari na kwingineko. Utaratibu huu si wa chama chetu,” alisema Nape.
“Tunashauri taratibu zifuatwe. Katika kufikia hatua hii tunawaomba wanachama wawe watulivu.”
Alisema wanachama wamejaa mjini Dodoma wakijaribu kushawishi wajumbe kuhusu rufaa zao, lakini akasema kinachotakiwa kiwasilishwe ni malalamiko yao, ushahidi wa kutosha katika ngazi husika.”
Nape pia alisema kumezuka wimbi la matapeli linalowalaghai makada walioshindwa katika kura za maoni kuwa watoe fedha ili wawasaidie rufaa zao kwenye vikao hivyo.
Alisema matapeli hao wamesajili namba za simu za viongozi wa CCM na kwamba yeye ni mmoja wa viongozi walioathirika na utapeli huo kwa namba yake ya simu ya mkononi kutumika.
“Wanawataka kutoa fedha ili waweze kuwasaidia na tayari tumeshawanasa baadhi yao na kuwakabidhi polisi. Wawe makini wasikubali kutapeliwa fedha zao na kama wana malalamiko wafuate utaratibu uliowekwa,” alisema.
Pamoja na Nape kutotaja idadi ya rufaa zilizowasilishwa, Mwananchi iliongea na makada 16 ambao walithibitisha kuwa wanasubiri uamuzi wa vikao hivyo baada ya kutuma barua zao kupinga matokeo.
Mwananchi imeshuhudia makada waliobwagwa katika kura hizo, wakiwemo mawaziri wakiwa kwenye viunga vya jengo la makao makuu ya CCM mjini hapa.
Baadhi ya makada hao ni mbunge wa Busega, Dk Titus Kamani aliyeangushwa na Dk Raphael Chegeni. Kamani aliiambia Mwananchi kuwa amekata rufani kupinga matokeo ya kura za maoni kwa kuwa mchakato ulitawaliwa na rafu nyingi na anaamini yeye ni mshindi.
Mwingine aliyekuwa mjini hapa ni Juma Kilimba na David Jairo waliobwagwa Iramba Magharibi, Asumpta Mshama aliyeangushwa kwenye Jimbo la Nkenge.
Wabunge waliokata rufani
Vigogo wengine walioangushwa kwenye kura hizo ni Naibu Waziri wa Maji, Amos Makala (Mvomero), ambaye alisema amelazimika kukata rufaa baada ya kutoridhishwa na mchakato ulivyoendeshwa, ikiwa ni pamoja na baadhi ya viongozi wa CCM kutumika kumwangusha.
Alisema kulikuwa na hujuma wakati wa uchaguzi na baadhi ya viongozi wa chama walitumia mwanya huo kumjengea mazingira ya ushindi mpinzani wake.
Mbunge mwingine, Said Nkumba (Sikonge) alisema amekata rufani ili haki itendeke kwa kamati husika, baada ya kubaini kuwepo kwa njama za makusudi za kumwangusha hasa baada ya uongozi wa wilaya kuamuru upigaji wa kura urudiwe katika maeneo ambayo alionekana ameshinda. Madai kama hayo yalitolewa na Gregory Teu (Mpwawa) ambaye alikata rufaa akisema haki haikutendeka na kulikuwa na mchezo mchafu. Mbunge wa Dodoma Mjini, Dk David Mlole alisema ikiwa Kamati Kuu ya CCM itashindwa kuitendea haki rufaa yake, ataachana na masuala ya siasa.
Naye mbunge wa Morogoro Kusini –Mashariki, Dk Lucy Nkya alisema iwapo rufaa yake haitashinda, atakubaliana na matokeo na hatahama chama kwa sababu ya kushindwa katika kura za maoni.
Mshama alidai kuwa amehujumiwa katika mambo mengi yaliyojitokeza kwenye mchakato huo, ikiwamo baadhi ya washindani wake kupotosha kwenye vyombo vya habari kuhusu siku ya kura ya maoni.
“Jambo hilo liliwafanya baadhi ya wapigakura wangu kutojitokeza, hivyo kunifanya nikose kura zao. Nimefanya mambo mengi katika jimbo hili ambalo watu wake wanapenda elimu walinifurahia. Siamini kama wamenikataa, hizi ni hujuma,” alisema Mshama.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dk Titus Kamani alisema anavyojua ni kwamba yeye ndiye mshindi.
“Hivi wewe unaongea nini? Mimi najua nimeshinda sasa unasemaje nikuambie plan B yangu wakati nimeshinda mimi. Siwezi kushindwa na wala sijasikia kwamba nimeshindwa,’’ alisema Dk Kamani
Naye Nyambari Nyangwine, mbunge wa Tarime, alisema alisema mambo hayakuwa mazuri kwenye matokeo ya kura za maoni.
“Mimi siwezi kuhama chama kwani kutumikia wanaume wawili ni kazi kubwa. Unajua naamini Kamati Kuu itatenda haki tu,’’ alisema
Ally Kibona Mbunge wa Ileje alisema anaiomba CCM iwe makini na rafu ambazo zinachezwa ndani ya chama hicho hususan kipindi cha uchaguzi ikiwemo kuanza kampeni kabla ya muda wake.
Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mashariki mkoani Ruvuma, Gaudance Kayombo alisema kwamba yeye alishakata rufaa baada ya kutokubaliana na matokeo hayo ila hafikirii kukihama chama tawala.
Wakubali matokeo
Wakati makada hao wakisubiri kwa hamu uamuzi wa vikao vya juu vya chama, baadhi ya vigogo walioshindwa wamesema wamekubaliana na matokeo na hawana mpango wa kukata rufaa.
Wabunge hao ni pamoja na Dastan Mkapa (Nanyumbu), Dk Muhammed Seif Khatibu (Uzini), Mathias Chikawe (Nachingwea), Gaudensia Kabaka, Adam Malima (Mkuranga) na Salehe Pamba (Pangani).
Vikao vya uteuzi
Nape alisema jana kuwa vikao vya Taifa vya chama hicho vilianza jana na sektarieti itakaaa kwa siku mbili, ikifuatiwa na Kamati Kuu ya Taifa na Halmashauri Kuu itakayokutana Jumatano na Alhamisi.
“Kwa nafasi ya ubunge na uwakilishi tunategemea kufanya uteuzi Agosti 8 (Alhamisi),”alisema Nape.

Post a Comment

 
Top