Rais wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete amesema kwamba maarifa mafupi ya viongozi CCM ndio kikwazo kikubwa cha chama kushindwa kujipatia kipato kutokana na kuwa rasilimali nyingi mfu kuliko chama chochote cha siasa nchini Tanzania ambazo hazijaweza kukizalishia chama kipato. Kikwete amesema hayo leo wakati akizindua jengo jipya la CCM lilipo barabara ya kwenda chuo kikuu cha Dodoma ambalo limejengwa mahusisi kwa ajili vikao vya chama pamoja na chama kujiongezea kipato kutokana na kulikodisha jengo hilo kwa matumizi mengine. “Ukumbi huu utatumika mara mbili tu kwa mwaka hivyo hautakaa tu usubiri vikao hivyo, utakodishwa kwa watu wengine ambao watailipa CCM”.Amesema Rais Kikwete. Ameongeza kuwa CCM ina rasilimali nyingi ikiwemo viwanja katika maeneo mbalimbali nchini, rasilimali hizo zimekuwa zikigawanywa kwa viongozi wa mikoa pamoja na mapato yake kutia mfukoni. Ametolea mfano jijini la Dar es salaam CCM ina viwanja taribani 420 ambavyo havija endelezwa na matokeo yake kutumika kulazia magari na walinzi kujichukulia mapato yanayopatikana. Amewataka viongozi wa chama hicho kuingia ubia na makampuni ya ujenzi ili kuendeleza maeneo hayo kwa mkataba utakao zinufaisha pande zote mbili. Amesisitiza kuwa viwanja vya CCM sasa vibadilike kutoka rasilimali mfu hadi kuwa rasilimali zinazotoa na kukuza mtaji. Ukumbi huo una uwezo wa kuchukua wajumbe takribani 3000 ukiwa na ukumbi mkubwa pamoja na kumbi nyingine ndogo ndogo huku ukiwa na sehemu pana ya maegesho ya magari.
|
Post a Comment