0


Ugonjwa wa Saratani ya Tezi Dume umetajwa kuwa ndio chanzo kilichopelekea kifo cha Spika Mstafuu wa Bunge la Tanzania, Samwel John Sitta.

Mtoto wa marehemu Samwel Sitta, Benjamin Sitta ambaye ni Meya wa Manispaa ya Kinondoni alisema kuwa baba yake alifariki kutokana na saratani ya tezi dume ambayo ilikuwa imesambaa mwilini kiasi cha kumfanya ashindwe kutembea.

Samwel Sitta alifarika alfajiri ya jana nchini ujerumani alipokwenda kwa ajili ya kupatiwa matibabu ikiwa ni kwa mara ya pili kwenda nchini humo baada pia ya kwenda India kwa ajili ya matibabu.

Wataalamu wa afya wameeleza kuwa ugonjwa huu huwaathiri zaidi wanaume wengi wenye umri kuanzia miaka 60. Aidha, wameeleza kuwa tezi dume hupatikana chini ya kibofu cha mkojo na imezungukwa na mirija ya mkojo.

Mbali na watu wenye umri kuanzia miaka 60, watu wengine walioko kwenye hatari ya kupata ugonjwa huu ni pamoja na wanaume kutoka Afrika (Weusi), wanaume ambao kwenye familia zao kuna historia ya ugonjwa huu.

Saratani hii hupelekea maumivu makali ya mifupa kwenye nyonga, mapajani na kiunoni, uume kushindwa kufanya kazi, kupungua uzito, uchovu, kichefuchefu, baadhi ya sehemu za mwili kushindwa kufanya kazi.

Kuna vipimo vya aina tatu vya saratani ya tezi dume ambapo, vipimo vya kwanza ni vile ambavyo hufanyika kuangalia kama mtu ana ugonjwa huo, vipimo vya pili hufanyika kuthibitisha kama ni saratani ya tezi dume au ni uvimbe tu, na vipimo vya tatu hufanyika kuangalia madhara yaliyosababishwa na ugonjwa huo.

Matibabu yake hufanyika ambapo mgonjwa akiwahi hospitali, tezi hizo huondolewa ili kuizuia saratani kusambaa zaidi mwilini, huweza pia kupatiwa tiba ya miozi, dawa.

Inashauriwa na wataalamu wa afya kuwa, kwa wanaume wote wenye umri kuanzia miaka 50 wafanye vipimo ili kuweza kufahamu kama wana saratani ya tezi dume au la.

Post a Comment

 
Top