0





MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imepokea maombi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ya kupandisha gharama za umeme kwa asilimia 18.19 kuanzia mwaka ujao.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imeeleza kuwa Oktoba 4, mamlaka hiyo ilipokea ombi la mabadiliko ya bei ya umeme, hivyo unaandaliwa mkakati wa kukusanya maoni ya wadau wa nishati hiyo.

“Mikutano ya ukusanyaji maoni kuhusu bei inayopendekezwa na Tanesco itaanza Novemba 16 katika mikoa ya Mwanza, Mbeya, Arusha, Dodoma  na kwa Dar es Salaam ni Novemba 23,” inaeleza taarifa hiyo.

Aprili mwaka huu, Tanesco ilituma maombi kwa Ewura ya kupunguza gharama za umeme kwa asilimia 1.1, lakini baada ya mamlaka hiyo kupitia maombi hayo, ilipunguza gharama hizo kwa asilimia 1.5 hadi 2.4.

Bei ya sasa baada ya punguzo hilo la Ewura kwa wateja wa shirika hilo, kutoka kundi la D1 wanaotumia kiasi cha umeme kuanzia kilowati 0 hadi 75 ni Sh 100 na zaidi ya kilowati 75 kwa mwezi wanatozwa Sh 350 kwa uniti moja.

Aidha, kwa wateja wa kundi la T1 ambao ni kuanzia majumbani, viwandani na biashara ndogo ndogo hutozwa kiasi cha Sh 292 kwa uniti moja na kwa wateja wa kundi T2 ambalo ni kundi linalotumia umeme kuanzia kilowati 7,500 hutozwa kwa wastani wa Sh 15,004 kwa mwezi kwa uniti moja.

Kwa makundi ya T3 na T4 wanaotumia umeme mkubwa kama vile kwenye machimbo, viwanda vikubwa na Mamlaka ya Umeme Zanzibar (ZECO) yenyewe hutozwa kiasi cha Sh 13,200 hadi 16,550 kwa mwezi kwa uniti moja.

Hata hivyo, kutokana na ombi hilo la ongezeko la bei kwa asilimia 18.19, sasa wateja wa kawaida wanaotumia umeme kuanzia kilowati hadi 75 watakuwa na ongezeko la Sh 18 ambapo endapo ombi hilo likiridhiwa watatozwa Sh 118 kwa uniti moja.

Aidha, kwa wateja wanaonunua umeme zaidi ya kilowati 75 ambao kwa sasa wanatozwa Sh 350 kwa uniti moja, endapo ombi hilo likipitishwa watakuwa na ongezeko la bei la Sh 63 hivyo watatozwa kiasi cha Sh 413 kwa uniti moja.

Kwa upande wa wateja wa kundi la T1 ambao ni kuanzia majumbani, viwandani na biashara ndogo ndogo wanaotozwa kwa sasa kiasi cha Sh 292, watakuwa na ongezeko la Sh 52.56 hivyo endapo ombi hilo litaridhiwa bei hiyo itapanda na kufikia Sh 344.56 kwa uniti moja.

Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo pamoja na kuthibitisha mamlaka hiyo kupokea maombi hayo, alisisitiza kuwa bado ombi hilo linachambuliwa na kufanyiwa tathmini na mamlaka hiyo kabla ya kuidhinishwa.

Post a Comment

 
Top