Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki, jana alishindwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili kujibu mashitaka ya uchochezi huku mdhamini wake akiieleza mahakama kuwa, yupo jijini Mwanza akisimamia kesi ya Esther Bulaya, Mbunge wa Bunda katika Mahakama Kuu ya Mwanza.
Lissu ambaye pia ni wakili wa Mahakama Kuu na mwansheria mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo anashitakiwa kwa uchochezi pamoja na washitakiwa wengine ambao ni ni Jabir Idrissa, mwandishi mwandamizi wa Gazeti la MAWIO, Simon Mkina, mhariri wa Gazeti hilo na Ismail Mehboob, meneja wa kampuni ya uchapishaji magazeti ya Flint.
Mdhamini wa Lissu, Ibrahim Hemed, alitoa taarifa ya kutofika kwa mdhamana wake mahakamani hapo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Ibrahim alidai kwamba Lissu amempatia taarifa kuwa ameshindwa kufika kwa sababu yupo kwenye kesi ya uchaguzi huku Peter Kibatala wakili wa utetezi akiiomba mahakama ipokee taarifa za Lissu na ikubali kuhairisha kesi hiyo.
“Lissu ni wakili pekee wa mlalamikiwa Esther Bulaya katika kesi ya uchaguzi,”alisema Kibatala.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Hakimu Simba aliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 31 mwaka huu.
Katika kesi hiyo Lissu anaunganishwa kama mshitakiwa kufuatia kunukuliwa akitoa maoni yake katika habari iliyochapishwa na gazeti la MAWIO ikiwa na kichwa cha habari “Machafuko yaja Zanzibar.”
Post a Comment