TIMU ya Stand United imeweka rekodi msimu huu kwa kucheza michezo sita pasipo kupoteza, ikishika nafasi ya pili nyuma ya vinara Simba inayoshika nafasi ya kwanza bila kufungwa pia. Stand United inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 12 na Simba ikishika nafasi ya kwanza kwa pointi 16.
Rekodi hiyo wamejiwekea baada ya kuifunga Yanga katika mchezo wa juzi bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kambarage Shinyanga na kuishusha timu hiyo ya Jangwani hadi nafasi ya tatu ikiwa na pointi 10 baada ya kucheza michezo mitano.
Katika ligi ya msimu uliopita, mpaka kufikia raundi ya sita Stand ilikuwa na pointi tisa ambapo ilipoteza mechi tatu na kushinda tatu.
Alipoteza dhidi ya Simba, Azam na Mtibwa Sugar na kushinda dhidi ya African Sports, Mbeya City na JKT Ruvu.
Licha ya timu hiyo ya Shinyanga kucheza kwenye mazingira magumu kwenye ligi ya msimu huu baada ya mfadhili wao Kampuni ya Acacia kujitoa walicheza soka nzuri na kuibuka na ushindi.
Kwa msimamo mzima wa ligi ni timu hizo mbili pekee hazijafungwa hata mchezo moja zaidi ya kushinda na kutoka sare. Katika michezo minne kati ya sita iliyocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani Stand United ilishinda dhidi ya Yanga bao 1-0, ikaifunga JKT Ruvu mabao 2-1, ikaifunga Toto Africans bao 1-0 na kupata sare dhidi ya Mbao 0-0.
Katika michezo yake mingine ikiwa ugenini Stand ilicheza na Mwadui na kupata sare ya mabao 2-2 kabla ya kutoka sare ya bila kufungana na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba. Simba imeshinda mechi tano na kutoka sare moja kati ya hizo mechi mbili za ugenini na nne za nyumbani.
Timu nyingine kama Yanga, Mtibwa Sugar, Prisons, Ndanda, African Lyon na Kagera Sugar ndio zilizopoteza mchezo moja moja hadi sasa, zikishinda na kutoka sare michezo mingine. Pia Azam FC, Mbeya City, Ruvu Shooting, JKT Ruvu, na Mwadui zimepoteza michezo miwili kila mmoja, zikishinda nyingine na kutoka sare.
Wakati huo huo, Toto Africans na Mbao zimepoteza michezo mitatu, zikishinda mingine na kutoka sare huku Majimaji ikiongoza kwa kufanya vibaya, kwani haijashinda mchezo hata moja.
Post a Comment