chenge |
Lakini uchaguzi wa viongozi wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac), ulihusisha nafasi za makamu mwenyekiti pekee baada ya wabunge wa vyama vya upinzani, vinavyotakiwa kuziongoza, kususia.
Vyama hivyo vinataka vipewe uhuru wa kuchagua wenyeviti badala ya kuchaguliwa na uongozi wa Bunge. Licha ya wapinzani kususia, wabunge wa CCM waliendelea na uchaguzi huo ulioleta sura nyingi mpya.
Uchaguzi huo umefanyika baada ya Bunge kutangaza mabadiliko ya kamati hizo kwa kuunda mpya mbili, kubadilishwa majina na nyingine kuunganishwa baada ya Rais John Magufuli kupunguza idadi ya wizara kwa kuziunganisha.
Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja, ambaye alivuliwa uenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria kutokana na kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, amechaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa Kamati ya Sheria Ndogo. Kabla ya hapo, Ngeleja alijiuzulu uwaziri wa Nishati na Madini baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kubaini ufisadi kwenye wizara hiyo mwaka 2012.
Kamati hiyo itaongozwa Andrew Chenge, ambaye mwaka 2008 alijiuzulu uwaziri wa Miundombinu kutokana na kashfa ya ununuzi wa rada uliofanywa wakati akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mwaka jana, Chenge alivuliwa uenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge kutokana na kuhusishwa kwenye sakata la escrow.
Waziri mwingine wa Serikali iliyomaliza muda wake, Dk Mary Nagu amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji. Dk Nagu alikuwa Waziri Ofisi ya Rais- Uwekezaji na Uwezeshaji.
Aliyekuwa Waziri wa Tamisemi wa Serikali ya Awamu ya Nne, Hawa Ghasia amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, huku Josephat Kandege akichaguliwa kuwa makamu wake.
Kati ya mawaziri hao watatu, Dk Nagu na Ghasia ndiyo pekee waliokaa hadi Serikali ya Awamu ya Nne inaondoka madarakani Oktoba 25 mwaka jana.
Uchaguzi wa viongozi wa kamati za Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na ya Viwanda na Biashara ulitarajiwa kufanyika jana baada ya kukwama juzi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ya akidi kutotimia.
Msimamo wa Zitto
Akizungumzia hatua ya Ukawa kususia uchaguzi, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alisema hakuna sababu kulalamikia kamati kwa kuwa zote ni sawa na zinahusu kero za wananchi.
“Kamati zote za Bunge zina hadhi sawa ndani ya Bunge. Kila mbunge ana haki ya kuwa kwenye kamati yoyote ile na hakuna mbunge bora zaidi ya mwingine,” alisema mwenyekiti huyo wa zamani wa PAC na kiongozi wa ACT-Wazalendo.
“Kanuni zimeweka utaratibu wa uteuzi, ikiwamo maombi ya mbunge, uzoefu na ujuzi wa eneo husika. Wanaolalamika leo upangaji wa kamati, ndiyo usiku wa kuamkia jana (juzi) walimshinikiza Spika asiwapange mahasimu wao kisiasa kwenye kamati wanazoona wao ni nyeti.”
Zitto alisema ni unafiki uliopitiliza unapojenga hoja ya uzoefu, chaguo la mbunge na ujuzi wakati wenye sifa zote wanawapiga vita kwa sababu za kisiasa.
“Ni dhahiri kuwa mpangilio wa Kamati unajenga Bunge kibogoyo. Nilitahadharisha kutoka Bunge la Kumi na Moja lilipoanza kwamba, kuna dalili za Serikali kutaka kulidhibiti Bunge. Kumbukeni sarakasi za Dk Tulia Ackson ambaye sasa ni Naibu Spika. Hata hivyo, muhimu kuheshimu uamuzi wa Spika na twende kufanya kazi huko alikotupanga,” alisema.
“Serikali ni chombo cha mabavu, lazima kidhibitiwe na ndiyo kazi ya Bunge kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 63,” alisema Zitto.
Post a Comment