0
MWANAMUZIKI wa Hip Hop, Kalama Masoud ‘Kalapina’ aliyekuwa amewekewa pingamizi ya kuwania ubunge katika Jimbo la Kinondoni, ameshinda rufani yake katika Tume ya Uchaguzi na kwa sasa ni mgombea rasmi wa jimbo hilo.
Kalapina, ambaye pia ni mwanaharakati wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya alisema jana kuwa atazindua kampeni zake kesho katika soko la Tandale. Aliwekewa pingamizi na mgombea ubunge wa CCM, Iddi Azzan kwa madai hakukamilisha fomu za uchaguzi kwa vile hakuwa na wadhamini wa kutosha.
Kalapina alisema uamuzi huo wa Tume ya uchaguzi ni uamuzi sahihi na kuwa tume hiyo imetenda haki kwa kumrejesha tena kwenye kinyang’anyiro. Alitoa mwito kwa wananchi kuhakikisha kuwa wanamchagua kwa kuwa anazo sera nzuri zenye kusaidia maendeleo ya jimbo hilo.
Alisema atasaidia michezo na sanaa kwa ujumla kwa kuwa anaamini kwa kufanya hivyo itasaidia kuongeza wigo wa ajira kwa vijana. Alisema: “Wananchi wanichague ili niwahudumie kwa kuwa ninayo nia na uwezo wa kufanya hivyo kwa kuwa ninajua kero zao na mimi ni mtoto wao na pia kijana mwenzao”.
Aliongeza kuwa atasaidia wananchi kujiajiri pamoja na kuwasaidia wananchi hao kufanya biashara mbalimbali ndogondogo ili kuwasaidia waendelee kimaisha. Alisema kuwa kama msanii wa muziki wa hiphop amekuwa akiimba kuhusu maisha kwa ujumla hasa akipambana na dawa za kulevya na kila aina ya shughuli mbaya kwa maendeleo ya wananchi.

Post a Comment

 
Top