0
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana.
Wanazuoni na wachambuzi wa masuala ya kisiasa wameichambua kwa kutoa maoni tofauti timu ya kampeni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema timu ya CCM imeundwa na makada wenye uwezo mbalimbali wakiwamo wa kurusha makombora makali kwa upinzani.

Alisema: “Unaweza kuona kamati hii ilivyopangwa imekamilika kwa sababu kuna watu wa kutoa mapigo na wenye busara kama akina Kinana (Abdulrahman) wa kuweka mambo sawa.” Alisema kamati ya CCM imezingatia hali ya kisiasa nchini na nguvu kubwa ya upinzani iliyopo akiwataja baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wenye uwezo wa kurusha makombora kwa upinzani kuwa ni Nape Nnauye, Dk. Harrison Mwakyembe, Samuel Sitta na Livingstone Lusinde.

Mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Haji Semboja, alisema kamati hiyo itaweza kufanyakazi yake kwa urahisi kama mategemeo ya wananchi katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, ulizingatia maslahi ya umma.

Alisema pia kuwa timu hiyo ina jukumu kubwa la kuushawishi umma umchague mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, kwa kuwa anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Edward Lowassa, anayepeperusha bendera ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

“Wananchi wanataka mabadiliko na wanaamini kuwa Magufuli na Lowassa ni watendaji wazuri kwa hiyo wananchi wanahitaji kujua ni kwa namna gani rais ajaye atatekeleza changamoto zinazowakabili …siyo suala la sera wala sheria kwa sababu tayari zipo nzuri,” alisema.

Dk. Semboja alisema kampeni za mwaka huu zinahitaji wagombea na timu zao kuzungumzia matakwa ya wananchi badala ya matusi au kejeli.

Bashiru Ali kutoka UDSM, alisema uteuzi wa mwaka huu uliohusisha watu wa makundi mbalimbali utasaidia kuvunja makundi ndani ya chama tawala.

“Na hii itatimiza kauli ya CCM ya umoja ni ushindi,” alisema.

Naye Mhadhiri mstaafu wa UDSM, Prof. Gaudence Mpangala, alisema uwingi wa makada wanaounda timu ya kampeni ya CCM siyo kigezo cha kuibuka na ushindi, bali wazungumzie sera za chama chao na siyo kutoa kauli za kuchafuana.

Kamati hiyo ina wajumbe 32 wanaoongozwa na Katibu Mkuu, Kinana.CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

 
Top