0
MGOMBEA urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Pombe Magufuli na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan wanatarajia kuanza kampeni zao mkoani Rukwa wakitokea mkoani Katavi.

Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Rukwa, Clement Bakuli, aliliambia jana gazeti hili kuwa wagombea hao wanaopeperusha bendera ya CCM katika kinyong’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu kuwa wanatarajiwa kufika kesho mkoani Rukwa.

Alisema baada ya kuwasili Rukwa, wagombea hao watapokelewa katika kijiji cha Paramawe, Jimbo la Nkasi Kaskazini. Kwa mujibu wa Bakuli, wagombea hao watafanya mikutano ya kampeni katika kijjiji cha Mtenga na mjini Namanyere wilayani Nkasi, kisha msafara wao utaelekea katika kijiji cha Chala ili kusalimiana na wananchi.

Alisema Dk Magufuli na msafara wake wakitoka Chala wataelekea Matai yaliko Makao Makuu ya Wilaya ya Kalambo atakofanya na mkutano wa kampeni.

Alisema mgombea urais huyo na mwenza wake watafanya mkutano wa kampeni Mjini Sumbawanga na kisha atakutana na makundi mbalimbali ya kijamii.

Alisema, siku inayofuata Oktoba 26, msafara wa mgombea urais huyo utaondoka Sumbawanga mjini na kuelekea katika kijiji cha Mtowisa katika Bonde la Ziwa Rukwa, Jimbo la Kwela katika wilaya ya Sumbawanga ambako atakuwa na mkutano wa kampeni kisha ataondoka mchana kuelekea kijiji cha Nzoka mkoani Mbeya.

Post a Comment

 
Top