0
Dar/Moshi. Siku tatu baada ya Baraza Kuu la Chadema kuridhia kumpumzisha kwa muda Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa baada ya kutofautiana na Kamati Kuu kwa kumkaribisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kiongozi huyo amesema yupo salama na wakati mwafaka ukifika atazungumza ya moyoni.
Akizungumza kwa mara ya kwanza na gazeti hili tangu Chadema imkaribishe Lowassa na hatimaye kumpitisha kuwania urais kupitia muungano wa Ukawa, Dk Slaa alisema amekuwa akisikia mengi yakisemwa juu yake lakini yote yamekuwa yakimchekesha tu.
Hakuhudhuria vikao muhimu vya chama hicho na vile vya Ukawa, vikiwamo; wakati Lowassa akitambulishwa rasmi, akichukua fomu, kikao cha Baraza Kuu na juzi Mkutano Mkuu na hakuwa akipatikana kwa simu yake ya mkononi.
Wakati kimya kikitawala juu ya hatima yake, baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiandika kuwa amejivua uanachama Chadema.
Lakini jana alisema: “Naangalia mambo mengi yanayoendelea kwenye mitandao halafu ninacheka tu, usifikiri sifuatilii, nafuatilia kinachoendelea na ninabaki nikicheka.”
Kuhusu hatima yake kisiasa na madai ya kujiuzulu uanachama ndani ya Chadema, alisema hawezi kuzungumza lolote kwa sasa na atafanya hivyo wakati mwafaka ukifika. “Usijali wakati wangu wa kuzungumza ukifika nitasema tu, sasa hivi nawaachia mzungumze, lakini nitazungumza,” alisema.
Kadhalika, alipoulizwa kuhusu taarifa zilizozagaa kuwa maisha yake yapo hatarini kwa kuwa anatishwa, Dk Slaa alisema hata hilo pia atalizungumzia wakati mwafaka ukifika.
“Ndiyo hayohayo ninayosema, wala msijali nitazungumza wakati ukifika,” alisema na kusisitiza: “Nipo salama.”
Dk Slaa alisema kwa sasa yupo mapumzikoni nje ya jiji la Dar es Salaam ingawa hakutaka kueleza ni eneo gani.
Juzi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alifafanua tofauti iliyojitokeza kati ya Kamati Kuu ya Chadema na Dk Slaa wakati wa mchakato wa kumpokea Lowassa
Katika mkutano huo wa Baraza Kuu la Chadema, Mbowe alisema wamekubaliana katibu mkuu huyo apumzike kwa muda... “Nina hakika kwa tabia na hulka za Dk Slaa… kwa sababu anajua tunampenda na yeye anakipenda chama hiki, tunamwombea kwa Mungu ampe nguvu na ujasiri wa kuona kwamba kauli ya wengi ni kauli ya Mungu.”
Ndesamburo na siri nzito
Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo na makada wengine wa Chadema, jana walikwenda kuonana na Dk Slaa nyumbani kwake na kufanya naye kikao cha faragha.
Picha zilizomuonyesha Ndesamburo akiwa na Dk Slaa na makada wengine akiwamo Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Jaffar Michael, zilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii jana na kuibua mijadala.
Baadhi ya waliochangia mijadala hiyo walidokeza kuwa huenda Ndesamburo anayeheshimika ndani ya chama hicho alikwenda kujaribu kusawazisha hali ya mambo.
Mkuu wa Idara ya Habari wa Chadema, Tumaini Makene alikiri kuwa picha hizo ni halisi, baadhi zilipigwa juzi na nyingine jana mchana, lakini hakutaka kuingia undani wa mkutano wa wanasiasa hao.
Ndesamburo alithibitisha kukutana na Dk Slaa: “Ni kweli tulikwenda, kwani kuna tatizo gani? Si mzee mwenzangu? Halafu bado ni mwanachama wetu, hajatoka Chadema, hivyo tuna kila haki ya kwenda kumsalimia.”
Alipoulizwa kama alikwenda kumsihi Dk Slaa arejee kuendesha mapambano ya kuing’oa CCM, Ndesamburo alisisitiza kuwa walikwenda kumsalimia.
Michael alipoulizwa nia ya safari hiyo alijibu kwa kuuliza; “Dk Slaa ni katibu mkuu wetu kwani tunazuiwa kwenda kumsalimia?”
Dk Slaa aligombea urais mwaka 2010 na kushika nafasi ya pili baada ya Rais Jakaya Kikwete na ndiye aliyekuwa akitajwa kuwania tena nafasi hiyo kupitia Chadema na Ukawa kabla ya “kubadili gia angani” na kumteua Lowassa.

Post a Comment

 
Top