0
Mabegi mawili yaliyowekwa fedha zilizokamatwa DodomaKAMPUNI ya Quality Group ambayo Mtendaji Mkuu wake ni Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, imetoa ufafanuzi wa fedha sh.milioni 700 alizokutwa nazo mfanyakazi wa kampuni hiyo, Amit Kevalramani akiwa nazo mjini Dodoma wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Quality Group, Kevalramani aliwasili mjini Dodoma kwa ndege ya kukodi kutoka Dar es Salaam kwa ajili ya kupeleka fedha za kununua mahindi na mchele kwa Kampuni ya M/s Tanrice Grains & Pulses Limited ambayo ni kampuni tanzu ya Quality Group.

Kampuni hiyo imetoa ufafanuzi huo, baada ya baadhi ya vyombo vya habari nchini kuandika kuwa fedha hizo zilikuwa ni kwa ajili ya kutoa rushwa kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao walikuwa na jukumu la kumchagua mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu kupitia chama hicho.

"Kwa nini mtu ambaye amekabidhiwa na Kampuni ya Quality Group kiasi cha fedha ambacho ni sawa na dola za Marekani 321,000 tu, achukuliwe kwamba alikuwa anatenda kosa la jinai kuwa na fedha hizo kwa mujibu wa vyombo vya habari, wakati gharama ya kuihudumia klabu ya Yanga, kila
msimu wa ligi katika misimu mitano iliyopita kiasi hicho cha fedha ni kidogo mno, ikilinganishwa na kile kinachotolewa na Quality Group? Ilihoji taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa, Kevalramani Julai 10, mwaka huu alikuwa akutane na watu wenye kuhusika na manunuzi kutoka Kampuni ya M/s Tanrice Grains & Pulses Limited, na alikuwa amepanga kurejea Dar es Salaam kwa ndege ya saa 3:30 Jumamosi iliyopita.

"Habari hizi zilizotolewa na vyombo hivyo vya habari zilianzisha uvumi huo katika mitandao ya kijamii, ikiwa ni pamoja na kusambaza picha pamoja na simulizi za kuchekesha," ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kikao kati ya Kevalramani na kampuni hiyo tanzu ya Quality Group kilichelewa, ambapo mfanyakazi huyo alipewa tiketi nyingine ya ndege kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam, ambayo ingeondoka saa 10:30 Julai 12, mwaka huu.

Ilieleza kuwa saa 3:30 asubuhi, Kevalramani
aliondoka katika hoteli aliyofikia na wakati akielekea kwenye gari alilokuwa amekodishiwa, alivamiwa na wezi na katika mapambano yaliyotokea, begi moja lililokuwa na fedha lilichanika na hivyo kuwafanya Maofisa Usalama kufika mara moja katika eneo hilo.

"Baada ya kuona njama zao zimekwama, wezi hao wakajifanya kuwa wafuasi wa CCM waliokuwa wamepanga katika hoteli hiyo na kuanza kupiga makelele wakisema 'rushwa', jambo ambalo liliwavuta watu wa vyombo vya habari kwenda mahali hapo.

"Katika mkanganyiko huo, Jeshi la Polisi la Dodoma lilikuwa makini katika kufanya kazi yake ambapo lilizikusanya fedha zote na Kevalramani akahakikisha fedha zake zote zipo na zilikuwa salama.

"Kwa nini, katika matukio ya rushwa ambayo uhusisha pande mbili, yaani mtoaji na mpokeaji, vyombo hivyo vilimtaja 'mtoaji' pekee na simpokeaji? ilihoji taarifa hiyo.

Taarifa hiyo pia ilieleza kutokana na maombi yao, Jeshi la Polisi lilihakikisha, Kevalramani anawekwa mahali penye usalama ambako asingefikwa na tishio lolote la kuibiwa fedha hizo.

Ilieleza kuwa walifanya hivyo wakijua kwamba kutokana na habari zilizochapishwa katika vyombo hivyo vya habari kuhusu, Kevalramani na fedha hizo ilikuwa ni lengo la makundi ya majambazi na makundi ya kisiasa yaliyokuwa yamekata tamaa.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Kampuni ya M/s Tanrice Grains & Pulses Limited na Quality Group Limited, inatoa shukurani kwa Jeshi la Polisi Tanzania kwa utatuzi wa haraka wa suala hilo na linampongeza, Kevalramani kwa ushupavu wake wa kukabiliana na jaribio hilo la wizi.

Post a Comment

 
Top