0
Viongozi wa juu wa ChademaHATIMAYE  Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetoa Mwongozo uliokuwa unasubiriwa kwa muda mrefu kuhusu namna ya kuendesha zoezi la kura ya maoni katika ngazi ya udiwani nchi nzima. Anaripoti Deusdedit Kahangwa …. (endelea).
Kwa mujibu wa Mratibu wa Kanda Taifa, Mohamed Mtoi, Mwongozo huo unaotaja wajumbe wa vikao vya uteuzi katani pamoja na masharti ya kisheria kuhusiana na zoezi hili, unapaswa kuzingatia na watendaji wote wa Chadema Tanzania nzima.
Kwa mujibu wa Mwongozo huo, Kamati ya Utendaji ya Kata nidyo yenye jukumu la “kufanya uteuzi wa awali wa wagombea Udiwani.” Baadaye, uteuzi huo unapaswa kuthibitishwa na “Kamati ya Utendaji ya Jimbo” husika. 
Mwongozo huo unasisitiza kwamba, ni muhimu masharti ya akidi ya vikao vya uchaguzi kwa mujibu wa Katiba ya Chadema kuzingatiwa. Kulingana na “Ibara ya 6.2.2 (b) ya Katiba ya Chama ya mwaka 2006 akidi ya Kikao cha Uchaguzi ni 75%,” inasema mwongozo.
Mbali na kutaja wajumbe wa vikao vya uteuzi, mwongozo huo umefafanua masharti ya uteuzi kwa mujibun wa Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za mitaa (Udiwani) ya mwaka 1979 (The Local Authorities (Elections) Act 1979).
Kwa mujibu wa sheria hii, chini ya Kifungu cha 39, mtu anayetaka kugombea Udiwani  anapaswa kuwa na vigezo vifuatavyo: awe raia wa Tanzania, awe ametimiza miaka 21, awe mwanachama wa Chama cha Siasa, na awe mkazi wa Halmashauri ambapo uchaguzi wa Kata unafanyika. 
Mwongozo huo umewakumbusha watendaji wa Chama kuzingatia masharti ya kifungu cha 40 cha sheria hiyo.
Kulingana na kifungu hicho, mtu atapoteza sifa za kugombea udiwani ikiwa mtu huyo ana uraia wa nchi nyingine; au mtu huyo amethibitika kuwa ana matatizo ya akili kwa mujibu wa sheria; au mtu huyo amehukumiwa hukumu ya kifo au hukumu nyingine jela zaidi ya miezi sita; au amewekwa kizuizini kwa muda unaozidi miezi sita; au ni mbia au meneja wa kampuni ambayo imeingia mkataba na Halmashauri husika ambayo yeye anagombea; au ikiwa amezuiliwa kujiandikisha kuwa mpiga kura kwa mujibu wa sheria.
Vile vile, mwongozo huo umewakumbusha watendaji hao kuzingatia masharti ya kifungu cha 42(1) cha sheria hii.
Kwa mujibu wa kifungu hiki, mgombea lazima awe na wadhamini wasiopungua kumi; lazima awasilishe tamko lililosainiwa na Hakimu kuona kuwa anazo sifa na vigezo vya kuteuliwa kugombea; na lazima awasilishe tamko la msimamizi wa uchaguzi wadhamini waliomdhamini ni wapiga kura halali wa Kata anayogombea.
Sababu za kuwasilisha pingamizi dhidi ya mgombea wa Udiwani, kama zilivyotajwa katika kifungu cha 44 cha sheria hiyo, zimegusiwa pia.
Kwa mujibu wa mwongozo huo, mgombea anaweza kuwekewa pingamizi ikiwa taarifa za mgombea zilizopo kwenye fomu ya kuomba uteuzi hazijitoshelezi kumtambulisha; au ikiwa fomu yake ya uteuzi haiendani na taratibu za kisheria za uteuzi; au ikiwa kutokana na yaliyomo kwenye fomu ya uteuzi mgombea anakosa vigezo vya kuteuliwa; au ikiwa pingamizi dhidi ya mgombea liwasilishwe kabla ya saa kumi siku inayofuata mara baada ya siku ya uteuzi. 
Utaratibu wa Kufanya Vikao vya Kura ya Maoni Katani
Kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na chama, utaratibu wa kufanya vikao vya kura ya maoni ngazi ya madiwani ni kama ifuatavyo:
Kwanza, Katibu wa Kata atachambua fomu za wagombea na taarifa zao kwa ajili ya kuwasilisha taarifa kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji ya Kata. Pili, Taarifa ya Katibu wa Kata kuhusu wagombea itawasilishwa kwenye Kamati ya Utendaji ya Kata.
Tatu, Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Kata kama walivyoainishwa katika ibara ya 7.3.8 ya Katiba wataipokea taarifa hiyo. Nne, kama Mwenyekiti wa Kata ni mgombea, basi kikao kitaazimia kumteua Mwenyekiti mwingine wa muda ambaye si mgombea.
Tano, Katibu wa Kata atawasajili wajumbe wote wa kikao na watasaini karatasi ya mahudhurio.
Sita, Katibu wa Kata ataandaa karatasi za kupigia kura ya maoni zikiwa na majina ya wagombea wote, kila jina la mgombea likiwa na kisanduku cha kumwezesha mpiga kura kuweka tiki mbele ya jina la mgombea. 
Saba, Katibu Kata ataandaa fomu za matokeo zikiwa na nafasi kwa ajili ya wagombea na mawakala wao kusaini baada ya uchaguzi, ili baadaye aweze kuwasilisha fomu hizo kwa Katibu wa Jimbo wa Jimbo/Wilaya.
Nane, Katibu wa Kata ataandaa muhtasari wa kikao cha uteuzi wa mgombea udiwani na kuhakikisha unasainiwa na Mwenyekiti na Katibu wa kikao. Tisa, Katibu wa Kata atawasilisha taarifa ya uteuzi kwa Katibu wa Jimbo/Wilaya kwa ajili ya hatua zaidi.
Na kumi, Kamati ya Utendaji ya Jimbo/Wilaya itapokea, kujadili na kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea udiwani. 
Nyaraka zinazohitajika wakati wa uteuzi wa wagombea udiwani
Kulingana na mwongozo uliotolewa na chama, mchakato wa uteuzi wa wagombea udiwani utaongozwa na nyaraka zifuatazo: 
Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa1979; Kanuni za Uchaguzi za Mwaka 2010; Mwongozo wa Tume kwa vyama vya siasa na wagombea wa Udiwani, Ubunge na Urais; Maadili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015; Katiba ya Chama ya Mwaka 2006 Toleo la mwaka 2014; Mwongozo wa Chama Dhidi ya Rushwa; na Kanuni za Uchaguzi wa Kiserikali na ndani ya Chama kama zilivyorekebishwa mwaka 2012.
Nyaraka nyingine ni Fomu za kuomba uteuzi za wagombea wa Udiwani; Fomu za mahudhurio ya wajumbe kikao cha uteuzi/mapendekezo; Karatasi za Kura na majina ya wagombea; Karatasi za taarifa ya Matokeo; na Muhtasari wa kikao cha uchaguzi utakaoandaliwa na Katibu wa Kata na Jimbo/Wilaya.
Utaratibu wa kura za maoni udiwani viti maalum.
Vigezo vya uteuzi wa Wagombea Udiwani Viti Maalum navyo vimetajwa katika mwongozo huu. Kwa mujibu wa mwongozo huu, vigezo vya jumla vya uteuzi wa madiwani viti maalum ni ka aifuatavyo:
Kwanza, ni lazima mgombea awe mwanachama wa CHADEMA; lazima awe mwanachama wa BAWACHA;  na lazima awe amejaza fomu zitakazoandaliwa na BAWACHA Makao Makuu kwa ajili ya kuwatambua wagombea. 
Kwa mujibu wa mwongozo huo, kutakuwa na kamati ya kupitia, kuchambua na kuchuja majina ya wagombea udiwani viti maalum. 
Kamati hiyo ya mchujo itaundwa na ngazi mbili. Katika ngazi ya kwanza kutakuwepo na Sekretariati ya BAWACHA Wilaya/Jimbo. Na katika ngazi ya pili kutakuwepo na Kamati ya Utendaji ya Wilaya/Jimbo. Kamati hii itapewa vigezo kutoka ngazi ya Taifa na kila kigezo kitakuwa na alama zake kwa ajili ya kuiwezesha kamati kuwapata wagombea walio bora. 
Mwongozo huo unafafanua kwamba, idadi ya Viti Maalum katika Halmashauri husika itategemea maelekezo yatakayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa Halmashauri husika. 
Lakini, “kama Tume watachelewa kutoa idadi ya Viti Maalum katika Halmashauri husika, Mkutano Mkuu wa BAWACHA ngazi ya Wilaya utachagua Madiwani wa Viti Maalum kulingana na Kata zilizopo,” unasema mwongozo.
Mwongozo huo, unaonyesha mtiririko ufuatao katika mchakato wa kuwapata wagombea wa udiwani wa viti maalum:
Kwanza, Katibu wa BAWACHA wa Jimbo atachambua fomu za wagombea waliojitokeza. Pili, taarifa ya uchambuzi wa Katibu wa BAWACHA Jimbo itawasilishwa kwenye kamati ya uchuchaji ya Jimbo/Wilaya.
Tatu, taarifa ya Kamati ya Uchujaji ya Jimbo/Wilaya itawasilishwa kwenye Mkutano Mkuu wa BAWACHA Wilaya kwa ajili ya kupiga kura. 
Nne, Katibu wa BAWACHA wa Jimbo atawasilisha taarifa ya matokeo ya Mkutano wa Mkuu wa BAWACHA wa Jimbo/Wilaya uliofanya uchaguzi wa madiwani wa Viti Maalum kwenye Kikao cha Kamati ya Utendaji ya Jimbo/Wilaya, kwa ajili ya uthibitisho.
Tano, Katibu wa Jimbo/Wilaya ataandika barua ya kuwasilisha matokeo ya uteuzi wa Viti Maalum kwa Mratibu wa Kanda kwa ajili ya kuyawasilisha kwenye ofisi ya Katibu Mkuu. Na sita, Katibu Mkuu atawasilisha majina ya Viti Maalum kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi

Post a Comment

 
Top