SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limeishtaki polisi Kanisa la Ufufuo na Uzima, linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima kutokana na kuharibu miundombinu ya umeme katika maeneo ya shirika hilo Jumamosi iliyopita na kusababisha umeme kukatika kwa baadhi ya mikoa na Jiji la Dar es Salaam.
Kutokana na kukatika kwa umeme kwa muda huo, shirika limepata hasara ya zaidi ya Sh milioni 30 ambayo ni mapato kama kungekuwepo umeme mbali na usumbufu mwingine waliopata kama kuwasha mitambo upya.
Meneja Uhusiano wa Tanesco, Adrian Severin alisema shirika hilo limefungua jalada namba 4397/2015 dhidi ya kanisa hilo katika Kituo cha Polisi Kimara katika Manispaa ya Kinondoni kwa sababu hiyo.
Severin alisema kuwa Agosti 29, mwaka huu kuanzia saa tisa alasiri hadi saa 12 jioni, umeme ulikatika katika Jiji la Dar es Salaam na mikoa iliyoungwanishwa katika gridi ya Taifa.
Alisema baada ya uchunguzi wa kina waligundua chanzo cha kuzimika umeme siku hiyo ilikuwa ni hitilafu ya umeme iliyotokea eneo la Ubungo Chai Bora kwenye kanisa hilo la Askofu Gwajima.
“Watu wanaosadikiwa kuwa watumishi wa kanisa hilo walikuwa wakishusha kontena kwa kutumia crane (winchi) chini ya nyaya za umeme wakati wakinyanyua kontena hilo liligusa laini ya msongo mkubwa wa kilovoti 132 inayopeleka umeme Zanzibar,” alifafanua Meneja Uhusiano wa Tanesco.
Severin alieleza kuwa tukio hilo lilisababisha mlipuko mkubwa ulioambatana na kuzimika kwa kituo kikubwa cha kupoozea umeme na mitambo ya kuzalisha umeme iliyopo Ubungo jijini Dar es Salaam.
“Kukatika huko kwa umeme kuliathiri shughuli za uchumi na kijamii ikiwemo mikutano ya kampeni za siasa kwa baadhi ya vyama iliyokuwa unaendeleo katika Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine,” alisema ofisa huyo.
Siku hiyo ilikuwa na uzinduzi wa kampeni za urais za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na baadhi ya watu walihusisha tukio hilo kuwa ni makusudi na hujuma za kisiasa; jambo linalothibitika si kweli.
Meneja Uhusiano wa Tanesco alisisitiza kwamba kukatika kwa umeme siku hiyo, haikuwa makusudi au kwa nia ya kuhujumu vyama vya siasa, kama ambavyo imekuwa ikielezwa na baadhi ya watu kwenye vyombo vya habari na hasa mitandao ya kijamii.
Kwa upande wake, Askofu Gwajima alipoulizwa kwa simu kuhusu tuhuma hizo, alisema hana taarifa na ndiyo kwanza anazisikia kutoka kwa mwandishi, licha ya kuwepo taarifa za Tanesco kuonana na uongozi wa kanisa hilo na kuzungumzia jambo hilo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alisema hajapata taarifa hizo na atazifuatilia.
Post a Comment