0
POLISI mkoani Kilimanjaro imekanusha madai ya kumzuia mgombea urais anayeungwa mkono na vyama vinne vya upinzani vinavyounda kundi la Ukawa, Edward Lowassa, asihudhurie maziko ya mwanasiasa mkongwe, Peter Kisumo yaliyokuwa yakifanyika wilayani Mwanga.
Badala yake, imefafanua kuwa Waziri Mkuu huyo aliyejiuzulu kwa kashfa ya kampuni feki ya kufua umeme ya Richmond na viongozi wengine wa vyama vya upinzani, walisusa wenyewe kwenda katika maziko hayo, ambayo pia yalihudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete na viongozi wengine wa CCM na Serikali.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Fulgence Ngonyani, alifafanua kuwa askari wake walitoa maelekezo kwa Lowassa na wenzake, kutokwenda msibani na msafara wenye wingi wa magari na pikipiki, kutokana na ufinyu wa eneo la kuhifadhi vyombo hivyo, kwa kuwa ulitanguliwa na magari mengine.
Kwa mujibu wa Ngonyani, alipokea simu kutoka kwa mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia na mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, kwamba msafara wao ulioongozwa na Lowassa umezuiwa kwenda kijiji cha Usangi katika maziko hayo, akalazimika kutaka ufafanuzi kutoka kwa maofisa waliopo chini yake.
“Nilizungumza na Mkuu wa Upelelezi wa wilaya ya Mwanga, akanieleza msafara wa viongozi wa vyama vya upinzani una magari zaidi ya 70 na pikipiki zaidi ya 600, nilielekeza kuwa viongozi, wasaidizi na walinzi wanaweza kwenda lakini wengine hawatapata nafasi kutokana na ufinyu wa eneo,” alisema.
Baada ya maelekezo hayo, badala ya viongozi hao waliokuwa katika wilaya ya Mwanga kwenda katika maziko wakifuatana na wasaidizi na walinzi wao, waliamua kurudi Moshi na kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kurejea Dar es Salaam kuendelea na shughuli nyingine.
Kamanda Ngonyani alisema kabla ya hapo, Agosti 12 alipata tetesi kwamba katika maziko ya Kisumo, wangekuwepo viongozi wengine akiwamo Lowassa ambapo naye alihoji hilo kwa OC CID, ambaye alisema hana taarifa juu ya hilo.
“Kutokana na hilo nilimpigia Katibu wa Mbunge wa Moshi Mjini, Ndesamburo, Basil Lema kutaka kujua kama ujio huo ni wa kweli, ambapo alikiri na kusema atashukia KIA na kufafanua kuwa hapatakuwa na maandamano yoyote,” alisema.
Kamanda Ngonyani alisema pia Lema alikanusha madai kwamba Lowassa angepitia ofisi za Chadema kata ya Majengo katika manispaa ya Moshi, lakini pia alieleza kuwa msafara wa viongozi hao kwenda Mwanga, ungekuwa na magari machache.
Pamoja na kuhakikishiwa kwamba kusingekuwa na msafara mrefu, Kamanda Ngonyani alisema juzi lilipita gari la matangazo ya wazi, likihamasisha wananchi na wanachama wa Chadema kwenda kumpokea Lowassa, na baadaye alipowasili yalionekana magari yakiwa na bendera za Chadema yakiwa katika msafara kwenda Mwanga.
Hata hivyo, Polisi ilimkamata mtu aliyekuwa akitoa matangazo hayo na kumfikisha katika ofisi za manispaa ya Moshi ili kuhakiki uhalali wa kufanya matangazo ya wazi, kwani jambo hilo lipo chini ya mamlaka ya manispaa hiyo na baada ya hapo Polisi haikuingilia tena jambo hilo.
Kuhusu kutumia mabomu ya machozi kutawanya wananchi, Kamanda Ngonyani alisema Polisi ililazimika kutumia mabomu hayo katika eneo la Njia Panda ya Himo, baada ya viongozi wa vyama vya upinzani kutaka kufanya mkutano wa hadhara, ambao hauna kibali na ungeathiri shughuli za wananchi.
Alisema baada ya Polisi kutoa ilani ya kutofanyika kwa mkutano huo, viongozi na wafuasi wa vyama hivyo, walikaidi ilani hiyo na kuwalazimu kupiga bomu ili kuwatawanya jambo ambalo lilifanikiwa na hapakuwa na madhara kwa wananchi hao.
Katika hatua nyingine, kamanda huyo alikanusha taarifa zilizozagaa katika mitandao ya kijamii kwamba alizungumza na wanahabari kuhusu kuzuia msafara wa Lowassa kwenda msibani, huku pia akikana maelezo ya kupata shinikizo kutoka ngazi za juu kuhusu kuzuia msafara huo.
Alisema taarifa hizo, zimejaa upotoshaji na kutaka vyombo vya habari kuripoti taarifa sahihi, kwani kinyume na hapo huenda wakaleta uchochezi hususani kipindi hiki Taifa likielekea katika Uchaguzi Mkuu.

Post a Comment

 
Top