0


 WAKATI moto wa kampeni za Uchaguzi Mkuu ukipamba moto mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa amekuja na ahadi ya kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu. Lowassa ametoa kauli hiyo akihutubia mkutano wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho zilizofanyika katika uwanja wa Jangwani na kuhudhuriwa na maelfu ya wapenzi wa chama hicho pamoja na washirika wake.

Chadema ambayo inaungwa mkono na vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi pamoja na NLD katika uzinduzi huo imeeleza ilani yao kipaumbele cha kwanza hadi cha tatu ni elimu, kwani kinaamini Watanzania wakipata elimu bora safari ya maendeleo itakwenda haraka.

Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe alimkabidhi mgombea urais, Lowassa pamoja na mgombea mwenza ilani ya uchaguzi ya chama hicho na kuahidi itazungushwa takribani mikoa yote ikinadiwa.
Hafla hiyo ya uzinduzi wa kampeni za urais kwa Chadema ambazo pia zinaungwa mkono na vyama vine kupitia umoja na ushirikiano wa vyama vinavyounda UKAWA, iliohudhuriwa na viongozi wakuu wa vyama hivyo, ulipambwa na jumbe za mabango mbalimbali yaliyokuwa yameshikwa na wananchi.

Akifafanua zaidi mgombea, Lowassa baada ya kukabidhiwa ilani ya chama chake alisema vipaumbele katika ilani ya kuwa ni elimu, ambapo alieleza kuwa ili nchi iendelee ni lazima kuboresha elimu ikiwa ni pamoja na serikali kugharamia elimu hiyo kutoka darasa la kwanza hadi chuo kikuu jambo ambalo alijinasiku kuwa linawezekana wakiingia ikulu.

Aliongeza kuwa kipaumbele kingine ni Kilimo, ili kuweza kuleta ajira kwa Watanzania ikiwa ni pamoja na kusambaza zana za kisasa za kilimo na serikali kununua mazao kwa mkulima bila kuwakopa na endapo itakopa italazimika kulipa na riba.

Aidha amelitaja suala zima la afya, ambapo alisema watajenga hospitali vijjini na kuakikisha kunakuwepo na huduma bora za upasuaji bila kutegemea kwenda katika mataifa mengine jambo ambalo limekuwa likiigharimu kiasi kikubwa cha fedha.

Alisema kuwa ni lazima kuwe na mawasiliano thabiti ikiwa ni pamoja na kuifufua shirika la ndege la Tanzania kwani ni jambo la aibu kushindwa kuliendesha shirika hilo na kuliacha life. Alidai kinachotakiwa ni kulifanya shirika hilo kuwa la kibiashara zaidi.

Lowassa amesema kuwa suala la maji hasa vijijini ni suala lililopewa kipaumbele kwani ndiyo wanawake wengi hutumia muda mrefu kutafuta maji na kusababisha kudorora kwa shughuli za maendeleo.
Awali Mwenyekiti wa chama hicho Mbowe alisema mabadiliko hayatakuwa na maana kama hayataleta maendeleo kwa Watanzania, hivyo ni lazima maslahi ya raia yapewe kipaumbele, na waishi katika nyumba bora na siyo za tembe na kuwapa mwanga mpya wa maisha.

Alisema kuwa wanachama waliokihama Chama Cha Mapinduzi wameleta chachu kubwa kwa UKAWA kwani umoja huo unatamani Watanzania kuondokana na umaskini na kuishi maisha bora zaidi.
Aidha Mbowe amesema kuwa wao kama UKAWA wameridhika na Lowassa kwakua yeye ni chahcu ya maendeleo hana ubinafsi na si mnafiki na siku zote anapenda mabadiliko na kuongeza kua UKAWA watafanya kampeni safi zisizo na vurugu wala uvunjifu wa amani.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye alisema kuwa CCM wameendesha siasa za chama kimoja kwa kujivika ngozi za vyama vingi na kuwataka kuwaacha watanzania kufanya maamuzi yao bila kuwazonga kwani wakati wa mabadiliko ni sasa na waache kuwajaza woga kuwa watakapo chagua upinzani wataaharibu nchi.

Naye James Mbatia amewahakikishia Watanzaia wote wataishi katika maisha ya amani na maendeleo na kumtaka Rais Jakaya Kikwete kuachana na tabia ya uchochezi kwa taifa kwani watanzania ni wamoja na kufanya hivyo ni kuwagawanya na wao hawapo tayari kuona watanzania wakigawanyika.

Mwenyekiti wa kamati ya uongoozi CUF, Waziri Msimo yeye amewapongeza Watanzania kwa kupokea mabadiliko yatakayo wapeleka kwenye maisha bora ya kweli na UKAWA ndio jibu lao la kweli.

Naye Halima Mdee amewataka akina mama wote kujitokeza kwa wingi na kupiga kura kwani akina mama ni jeshi kubwa na ndio watakao leta mabadiliko ya kweli ikizingatiwa wao ndio wanaotaabika katika kupata huduma bora za afya na kusababisha vifo vya kinamama na watoto wakati wa kujifungua, huduma za maji, elimu na uchumi duni na kusema kuwa wakati ni sasa kwani wanawake ni jeshi kubwa na wanatakiwa kufanya mabadiliko. Uzinduzi huo ulikuwa na kauli mbiu ya “LOWASSA MABADILIKO, MABADILIKO LOWASSA”.
posted from Bloggeroid

Post a Comment

 
Top