Na Mwandishi Wetu
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha ya waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2015/2016 ambao fomu za maombi zimegundulika kuwa na upungufu na kuwataka kufanya marekebisho kabla au ifikapo tarehe 11 Septemba mwaka huu (2015).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bodi hiyo leo (Ijumaa, Agosti 28, 2015), jumla ya fomu za waombaji wa mikopo 7,788 kati ya 68,445 zilizopokelewa na kuhakikiwa zimegundulika kuwa fomu zina upungufu na kuwataka waombaji kusoma majina yao katika tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. George Nyatega, (Pichani) waombaji ambao fomu zao zimegundulika kuwa na upungufu wanatakiwa kurekebisha kabla au ifikapo tarehe 11 Septemba mwaka huu (2015).
“Baada ya kusitisha uombaji wa mikopo kwa njia ya mtandao kwa mwaka wa masomo 2015/2016, Bodi ilianza kufanya uchambuzi wa maombi yote yaliyopokelewa na kugundua kuwa maombi 7,788 ya mikopo yanakosa taarifa muhimu,” inasomeka taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, taarifa muhimu zinazokosekana ni pamoja na sahihi za waombaji, nakala za vyeti vya kuzaliwa vya waombaji, sahihi na picha za wadhamini na baadhi ya fomu za maombi kutosainiwa na wanasheria na maafisa wa serikali za mitaa kama maelekezo yanavyotaka.
“Bodi inawataka waombaji wa mikopo ambao fomu zao za maombi zimegundulika kuwa upungufu, kufika wao wenyewe katika ofisi za Bodi zilizopo Mwenge jijini Dar es Salaam ili kufanya marekebisho katika fomu hizo,” imesisitiza taarifa hiyo na kuongeza kuwa majina waombaji wanaotakiwa kufika katika ofisi za Bodi yanapatikana katika tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz).
Aidha, Bodi ya Mikopo imewakumbusha waombaji wa mikopo kuwa waangalifu na kuchukua tahadhari dhidi watu wasio waaminifu ambao wanaweza kutumia zoezi hilo kuwadai fedha.
HESLB ilianzishwa kwa sheria ya Bunge na 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005 ili, pamoja na majukumu mengine kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji waliodahiliwa katika taasisi za elimu ya juu.
Aidha, jukumu jingine la Bodi ni kudai na kukusanya mikopo yote iliyotolewa kwa wahitimu wa taasisi za elimu ya juu kuanzia mwaka 1994 wakati Serikali ilipoanza kukopesha wanafunzi.
Post a Comment