0
KWA UFUPI
Kikao hicho ni hatua ya pili baada ya kukamilika kwa kikao cha Kamati ya Maadili kilichokutana jana usiku chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete huku kikitawaliwa na usiri mkubwa, kuhama ukumbi na kila dalili za kubadili ratiba iliyopangwa awali ili kuvuruga mipango ya kambi za wagombea.

Dodoma. Kisu kikali cha Kamati Kuu ya CCM (CC) leo kitaondoka na vichwa 33 kati ya 38 vya walioomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho kumrithi Rais Jakaya Kikwete anayemaliza ngwe yake.
Kikao hicho ni hatua ya pili baada ya kukamilika kwa kikao cha Kamati ya Maadili kilichokutana jana usiku chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete huku kikitawaliwa na usiri mkubwa, kuhama ukumbi na kila dalili za kubadili ratiba iliyopangwa awali ili kuvuruga mipango ya kambi za wagombea.
Habari zilizolifikia gazeti hili zilisema kulikuwa na uwezekano wa kubadili ratiba ili vikao vya Kamati ya Maadili na CC ama vifuatane au vifanyike usiku ili kuyanyima makundi nafasi ya kujipanga.
Alipoulizwa jana kuhusu vikao hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alidai kuwa hata yeye hakuwa na uhakika wa lini na muda gani hasa kikao cha Kamati ya Maadili kingefanyika.
Awali, vifaa vya ukaguzi wa wajumbe vilikuwa vimewekwa katika Makao Makuu ya CCM, White House lakini baadaye jioni viliondolewa na hapakuwa na taarifa zozote zilizotolewa.
Habari zilizopatikana baadaye zilidai kuwa kikao hicho cha Maadili kilitarajiwa kufanyika Ikulu ya Dodoma kuanzia saa nne usiku wa jana.
Haya yanajitokeza wakati macho na masikio ya Watanzania yakiwa hapa Dodoma kusikiliza namna kazi ya kuchuja wagombea itakavyofanyika na kujua ni watu gani 33 watakaoanza kulambwa na kisu cha CC, hasa kwa majina makubwa yanayotazamwa na wengi, mara tu baada ya kujadiliwa na Kamati ya Maadili.
Kazi za Kamati Kuu leo
Kikao cha CC kina majukumu matatu leo ambayo ni kufikiria na kutoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), majina yasiyozidi matatu ya walioona kuwania urais wa Zanzibar ambayo imeombwa na Rais wa sasa, Dk Ali Mohamed Shein pekee, kufikiria na kutoa mapendekezo kwa NEC majina yasiyozidi matano ya walioomba kuwania urais wa Muungano na kuandaa mkutano wa NEC.
Vigezo vya maadili
Kulingana na kanuni za Uongozi na Maadili, toleo la 2012 kifungu cha 4(ii), kuhusu taratibu za kuomba uongozi, wanachama wanaogombea uongozi ambao uteuzi wao hufanywa na vikao vya kitaifa, watachunguzwa kwanza uadilifu wao na chombo cha maadili cha CCM kwa ushirikiano na vyanzo vingine.
Kanuni hizo zinasema mwanachama wa CCM anapoomba uongozi katika ngazi yoyote, itikadi na mwenendo wake vitachunguzwa kwanza na Kamati ya Usalama na Maadili inayohusika, ndipo maombi hayo yaliyoambatanishwa na mapendekezo ya kamati hiyo yatakapofikishwa mbele ya kikao chenye madaraka ya kutoa uamuzi.
mwananchi

Post a Comment

 
Top